Featured Kitaifa

KAMATI YA BUNGE YAIAGIZA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA NA TAASISI ZAKE KUONGEZA KASI NA UBUNIFU UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU

Written by mzalendoeditor

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji, Viwanda, Biashara na Mazingira yaiagiza Wizara na Taasisi zake  kuendelea kuongeza kasi na ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji, Viwanda, Biashara na Mazingira imeiagiza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara pamoja na Taasisi zake kuendelea kuongeza kasi na  ubunifu  katika utekelezaji wa jitahada mbalimbali za kuendeleza sekta hiyo ili kukuza uchumi  wa Taifa.

Hayo yamesemwa na  Mwenyekiti wa  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji, Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. David Mwakiposa Kihenzile (Mb) wakati  Wizara hiyo ilipowasilishaTaarifa  ya Utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka 2021/2022  ya Wizara na Taasisi zake kwa Wajumbe wa  Kamati hiyo, Machi 23, 2022  katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Aidha, Wajumbe wa Kamati hiyo walipata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali  yanayolenga kuboresha utendaji kazi na utekelezaji wa jitihada na mikakati mbalimbali ya kuendeleza  Sekta ya uwekezaji, viwanda na biashara ili kuongeza uwekezaji,  kukuza biashara na uchumi shindani wa viwanda.

Naye, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.)  aliihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara itayafanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa  ili kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara  na kutimiza malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuongeza ajira na  kukuza uchumi wa taifa.

Awali, akitoa Taarifa  ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Kamati hiyo pamoja na  bajeti ya Wizara, Katibu Mkuu  wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara alieleza kuwa Wizara imetekeleza majukumu mbalimbali katika mwaka wa fedha 2021/22  ambayo yameleta mafanikio makubwa katika sekta hiyo.

Prof. Kahyarara alielezea utekelezaji wa majukumu hayo ikiwemo uhuishaji wa Sera Sheria na Mikakati inayohusu uendelezaji wa sekta hiyo, uhamasishaji wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi, uendelezaji wa kongani za viwanda katika maeneo mbalimbali nchini, uboreshaji wa mazingira ya  uwekezaji na biashara, usimamizi wa viwanda vidogo na biashara ndogo,  uwezeshaji wa wananchi kiuchumi,  utekelezaji wa miradi ya kimkakati na uendelezaji wa mahusiano na majadiliano ya kibiashara baina ya nchi, kikanda na kimataifa.

Aidha, baadhi ya Wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo zilipata fursa ya kuwasilisha utekelezaji wa bajeti ya taasisi zao kwa mwaka wa fedha 2021/2022. Taasisi hizo ni pamoja na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Mauzo ya  Nje (EPZA), Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO).

Taasisi nyingine zilizowasilisha taarifa ya utekelezaji  wa bajeti zao kwa Wajumbe wa Kamati hiyo ni Pamoja Baraza la Ushindani (FCT), Wakala wa Vipimo (WMA )  Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo na Biashara ndogo (SIDO),  Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia vijijini ( CAMARTEC) na Shirika la Uhamdisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO).

About the author

mzalendoeditor