Uncategorized

WAZIRI BITEKO ATAKA WATUMISHI KUEPUKA VITENDO VYA RUSHWA

Written by mzalendoeditor

NA MWANDISHI WETU-WM
WAZIRI wa Madini, Dkt.Doto Biteko amezindua Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Madini huku akiwapongeza kwa namna ambavyo wanafanya kazi kwa ufanisi, hivyo kuwezesha mafanikio chanya nchini.
Dkt.Biteko alizindua baraza hilo Machi 23, 2022 mkoani Morogoro huku akirejea wito wake wa mara kwa mara kwa watumishi kuwa, wanapaswa kufanya kazi kwa uadilifu na kuepuka vitendo vya rushwa.
“Napenda kuushukuru kwa dhati uongozi wa wizara kwa kunipa heshima ya kuzindua Baraza la Wafanyakazi ambalo ni la pili kuundwa baada ya baraza la kwanza kumaliza muda wake wa miaka mitatu.
“Ninaahidi kushirikiana nanyi nyote watumishi wa wizara na taasisi zilizoko chini yake katika kuwezesha nchi yetu kunufaika na utajiri wa rasilimali madini ambazo Mungu ametujalia kuwa nazo kupitia mapato ya Serikali, ajira na fursa nyingine zinazoendana na utajiri huu,”amesema Dkt.Biteko.
Amesema, Sekta ya Madini ni moja ya sekta ambayo wasipokuwa makini, “tutanyooshewa vidole. Tupambane na rushwa kwani inadhoofisha utoaji huduma, inaondoa haki kwa wananchi na kuleta manung’uniko tufanye kazi kwa uadilifu.
“Wizara haitamvumilia mtumishi yoyote atakayebainika na kuthibitika kujihusisha na vitendo vya rushwa. Hakikisheni mnabeba dhamana hii na kutekeleza kikamilifu wajibu wenu kwa weledi na kwa kuzingatia maadili ya kitaaluma na ya utumishi wa umma,”amesema.
Pia amesema, ushirikishwaji wa watumishi mahali pa kazi unaongeza morali ya kufanya kazi, “kabla ya kuwalaumu jiulize unaowaongoza umewapa nini? Wanajua mipango? Miongozo? Sera? Ilani ya Uchaguzi? Baraza ndilo linaunganisha mawazo yaliyotawanyika ili yafanane. Mwenyekiti wa Baraza wasikilize wajumbe ili kuboresha mipango yetu bila watu kujiona duni.
“Msisahau kujadili namna ya kuimarisha ustawi wa wafanyakazi. Wakati wa kujitathmini ndani tujue kwamba wapo wengi wanatutathmini kutoka ndani na nje ya nchi.
“Nendeni mkawakumbushe watumishi mnaowaongoza hivi karibuni wizara inatimiza miaka 5 tangu kuanzishwa kwake, jifanyieni tathmini msibweteke na mafanikio yaliyopatikana, angalieni viashiria hatarishi mvifanyie kazi msirudi nyuma.“Ninawapongeza wafanyakazi wa wizara kwa mafanikio tuliyoyapata, hadi sasa tumefanikiwa kukusanya zaidi ya bilioni 406 kwa mwaka huu wa Fedha tunaoendelea kuutekeleza, kilichosababisha mafanikio haya ni mazingira mazuri ya biashara ya madini pamoja na kuwepo kwa Sheria nzuri ya madini,”amefafanua Waziri Dkt.Biteko.
Katibu Mkuu
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adolf Ndunguru amsema kuwa, umoja, mshikamano na bidii za watumishi hao zimewezesha kukusanya Shilingi Bilioni 406 kuanzia Julai 2021 hadi Februari 2022.
Pia amesema, mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeendelea kuimarika. “Agenda Kuu katika Mkutano wa Baraza hili ni kupitia na kujadili utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2021/2022 na kupitia makadirio ya Bajeti ya wizara kwa mwaka 2022/2023. Pia, wajumbe watapata nafasi ya kupitia taarifa ya mapato na matumizi ya Mwaka 2021/2022 na masuala ya kiutawala na utumishi ya mwaka 2021/2022.“Katika kipindi hiki mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umendelea kuimarika ambapo katika kipindi cha miezi tisa (Januari hadi Septemba 2021) mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la taifa uliongezeka hadi kufikia asilimia 7.3 kutoka mchango wa asilimia 6.5 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2020.
“Katika robo ya Tatu Julai- Septemba 2021, Sekta ya Madini imechangia asilimia 7.9 ya Pato la Taifa, Mwelekeo unaonesha kuwa malengo yetu ya kuhakikisha sekta hii inachangia asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025 kama ilivyo matakwa ya Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2025 na Mpango wa tatu wa Maendeleo ya Taifa yanatekelezeka kila mtu akitimiza wajibu wake.
“Katika kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi kufikia Februari 2022, tumefanikiwa kukusanya maduhuli ya shilingi bilioni 404.6, sawa na asilimia 62.6 ya lengo la makusanyo.“Katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2021 hadi Februari 2022, wizara kupitia Tume yaMadini ilitoa jumla ya leseni 6,382 zikihusisha leseni za utafutaji wa madini, uchimbaji madogo, uchimbaji wa kati, uchimbaji mkubwa, uchenjuaji wa madini, usafishaji madini na biashara ya madini,”amesema.
Amefafanua kuwa, kupitia STAMICO imewezesha mafunzo na huduma mbalimbali kwa wachimbaji wadogo wapatao 1,144 waliotembelea vituo vya mfano vya Katente, Lwamgasa na Itumbi.
“Tumendelea kutangaza fursa zilizopo katika Sekta ya Madini kupitia mikutano ya kitaifa, kikanda na kimataifa ukiwemo mkutano wa kimataifa tulioandaa mwezi februari 2022. Tumeboresha Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji.
“Katika kuboresha ukusanyaji maduhuli, wizara imeanzisha mfumo wa kukusanya maduhuli ya madini ujenzi katika Mikoa ya Dar es salaam, Morogoro na Dodoma na unatarajiwa kutumika nchi nzima.
“Pamoja na mafanikio niliyoyataja, wizara inakabiliwa na changamoto za uwepo wa shughuli za utoroshaji wa madini zinazosababisha upotevu wa mapato ya serikali, uelewa mdogo wa wachimbaji, wafanya biashara wa madini na umma kwa ujumla kuhusu Sheria ya madini, hivyo kusababisha uwepo wa migogoro ya mara kwa mara,”amesema Nduguru.
Aidha, ili kukabiliana na changamoto hizo,amesema wizara imeweka mikakati na hatua mbalimbali ya kukabiliana nazo ikiwemo kuimarisha usimamizi wa shughuli za madini na ukusanyaji wa mapato ya serikali yatokanayo na wasilimali madini kwa kushirikisha mamlaka mbalimbali.
“Wizara imeendelea kutoa elimu na mafunzo ya mara kwa mara kwa wadau mbalimbali katika maeneo ya wachimbaji wadogo pamoja na viongozi wa Serikali za Mitaa kwa kuwajengea uelewa kuhusu dhana nzima ya kufuata Sheria ya Madini na Kanuni zake ili kuepuka migogoro,”amefafanua Katibu Mkuu huyo.
TUGHE
Naye Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Wizara ya Madini, Joseph Ngulumwa amesema kuwa, wanaushukuru uongozi wa wizara kwa namna ambavyo wamekuwa wakiwezesha watumishi kuhudhuria mafunzo mbalimbali.
“TUGHE tunatoa shukrani za dhati kwa uongozi wa wizara kwa kuendelea kuwezesha watumishi kuhudhuria mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwani mafunzo haya yanasaidia kuongeza weledi na ufanisi katika kazi za wizara.“Katika kuongeza uwezo wa watumishi, tunashauri watumishi kupatiwa uzoefu katika nchi zilizoendelea katika shughuli za uchimbaji madini na utafiti wa madini kama Australia, Canada na mataifa mengine yaliyoendelea. Aidha, tunashauri kuweka bajeti ya kusomesha wataalam nje ya nchi katika Shahada za Uzamili na Uzamivu walau watumishi 5 kwa mwaka.
“TUGHE inatambua kuwa michezo ni sehemu ya kuboresha afya kwa watumishi hivyo, Uongozi wa TUGHE unashauri wizara kuwezesha watumishi kushiriki michezo mbalimbali mfano SHIMIWI na BONANZA kwa kuwa na bajeti ya kutosha na kushiriki vema.
“Kwa niaba ya wafanyakazi, tunaomba suala la wafanyakazi bora kuongeza idadi kutoka mtumishi mmoja kuwa watumishi wawili kwa kila Idara na Kitengo ili kupanua wigo wa motisha kwa watumishi,”amesema Mwenyekiti huyo.
Katibu TUGHE
Wakati huo huo, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma, Samwel Nyungwa amesema kuwa,kuna umuhimu mkubwa wa watumishi kujiunga na TUGHE.
“Watumishi jiungeni TUGHE. Nawahamasisha watumishi kujiunga na Chama Cha Wafanyakazi. TUGHE ina lengo la kuratibu mahusiano kati ya Mwajiri na wafanyakazi ili kufikia lengo la kuboresha ufanisi mahali pa kazi.
“Mwaka huu Sherehe za Mei Mosi zitafanyika Kitaifa Mkoani Dodoma, tunategemea ushiriki mkubwa wa watumishi, niwaombe mjitokeze kwa wingi. Namshukuru Mwenyekiti wa Baraza kwa kuwa kikao kimekuwa na uhuru mkubwa. Mnapaswa kuwa na Semina na Mafunzo kwa wajumbe wa Baraza.
“Kutokana na namna mgeni rasmi alivyozungumzia suala la rushwa katika Sekta ya Madini, wakati mwingine alikeni wataalam kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na wanaohusika na masuala ya maadili ili wawafundishe,”amesema.

About the author

mzalendoeditor