Featured Kitaifa

WAZIRI JAFO:’MSINGI BORA WA UTUNZAJI WA MAZINGIRA UANZIE NGAZI YA WATOTO’

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Seleman Jafo akipanda mti wakati wa uzinduzi wa kampeni ya soma na mti aliyofanyika katika shule ya msingi Sinza Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Seleman Jafo akishiriki zoezi la upandaji miti kwenye kampeni ya soma na mti iliyofanyika katika shule ya msingi Sinza Jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Heri James akishiriki kwenye kampeni ya upandaji miti ya soma na mti iliyofanyika katika shule ya msingi Sinza Jijini Dar es Salaam.

Balozi wa mazingira Winfrida Shonda akizungumza na wanafunzi wakati wa kampeni ya soma na mti iliyofanyika katika shule ya msingi Sinza  Jijini Dar es Salaam.

Sehem ya wanafunzi wa shule ya msingi Sinza walioshiriki kwenye kampeni ya soma na mti iliyofanyika katika shule ya msingi Sinza Jijini Dar es Salaam

…………………………………………………………

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewaelekeza wakuu wa Mikoa, Wilaya na maafisa mazingira wote kuendelea kusimamia ajenda ya usafi wa mazingira na kusisitiza kuwa kila mwanafunzi apande mti mmoja kwani ndio msingi bora wa utunzaji wa mazingira.

Aliyasema hayo alipokuwa anazindua rasmi kampeni ya upandaji miti katika shule ya msingi Sinza iliyopo wilaya ya ubungo, Mkoani Dar es salaam. Aliendelea kusema kuwa maelekezo ya Rais mama Samia Suluhu Hassan ya upandaji miti, utunzaji wa mazingira na ufanyaji wa usafi lazima yafanyike kwa nguvu zote kwani Rais amepata heshima kubwa duniani hasa ya kimazingira kama Serengeti, Ngorongoro nk. Ambayo wengine hawana lakini pia nchi imeweka kielelezo kutengeneza miradi ambayo inajali mazingira kwa ajili ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

‘‘Watanzania wenzangu tujali sana ajenda ya mazingira na tupambane na mabadiliko ya tabia nchi, Natumia fursa hii kuwaomba watanzania na walimu wote twendeni tukapande miti. Tukipandakiza ajenda hii kwa Watoto watakuwa na ajenda ya kutunza mazingira katika Maisha yao yote, Tuna Halmashauri 184 na maelekezo ya Serikali ni lazima kila Halmashauri ipande miti milioni 1.5 wataalamu wa misitu kutoka TFS wanasema asilimia 62 huwa inastawi na lengo hilo likitimia Nchi yetu tutaifanya iwe ya kijani na Tanzania itakuwa salama.’’-alisema Dkt.Jafo

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Ubungo Bw. Herry James alisema kuwa Wilaya ya Ubungo inatekeleza kwa viwango maelekezo ya Serikali lakini pia inajali na kuheshimu mahitaji na maslahi ya wananchi wote ili kuwahudumia kwa uzuri na usalama ni lazima mazingira yao yawe safi wakati wote.

‘‘Sisi kama wana Ubungo tumepokea kampeni ya upandaji miti kwa mikono miwili. Na swala la utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti tutarithisha kuanzia kwa watoto shule,  mtoto huyu ambae yupo darasa la kwanza akikabidhiwa mti wake chini ya kampeni hii maana yake atamwagilia kwa kuutunza kwa miaka saba, siku anahitimu anapatiwa cheti cha kuhitimu na atakuwa anatukabidhi mti wetu alioutunza kwa miaka saba. Program ikisimamiwa vizuri tunao uhakika wa kuwa na miti ya kutosha na iliyotunzwa vizuri.’’- alisema Bw. Herry

Naye meneja wa Kanda ya Kaskazini Mashariki kutoka NEMC Bw. Arnold Mapinduzi amesema kama NEMC wameshiriki katika uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti ambao umeandaliwa na mabalozi wa mazingira lakini kama NEMC watakuwa wanakagua na kuhakikisha miti inakuwa na inaishi. Lakini kubwa ni kuwekeza kwa Watoto kunakuwa na uhakika zaidi wa uendelevu kwa familia na jamii kwa ujumla.

Balozi wa Mazingira Bw. Peter Niboye Amesema kama mabalozi wamejipanga kufanya kampeni hii ya upandaji miti nchi nzima na wapo tayari kupokea maelekezo na litakuwa ni zoezi endelevu.

About the author

mzalendoeditor