Featured Kitaifa

WANAFUNZI WA KITANZANIA UKRAINE WARUHUSIWA KUVUKA MPAKA WA RUSSIA

Written by mzalendoeditor

Wanafunzi wa Kitanzania walio katika mji wa Sumy nchini Ukraine wameruhusiwa kutoka nchini humo kupitia mpaka wa Russia baada ya mazungumzo ya kidiplomasia kufanyika na Serikali ya Russia kuridhia.

Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa jana Machi 4, 2022  na Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden na Ubalozi wa Tanzania nchini Urusi, shughuli ya kuwatoa wanafunzi wote kutoka Sumy hadi kwenye mpaka wa Russia, litaratibiwa na Serikali hiyo na tayari imeanza mipango ya utekelezaji.

“Wanafunzi hao watakapofika mpakani, Ubalozi wa Tanzania nchini Russia utawapokea kwa taratibu nyingine za kurejea nyumbani,” inaeleza taarifa hiyo ya Balozi hizo.

Taarifa hiyo inaeleza kwamba wakati shughuli ya kuwatoa wanafunzi walioko Sumy ikiendelea  kuratibiwa, Balozi zinaomba wanafunzi hao pamoja na wazazi kuwa wavumilivu ili kuhakikisha wanatoka kwa usalama nchini Ukraine.

About the author

mzalendoeditor