Featured Kitaifa

SERIKALI YAWAANGUKIA MACHIFU,WAZEE WA KIMILA KUHUSU MAUAJI

Written by mzalendoeditor

Baadhi ya Wazee wa Kimila Mkoani Tabora wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian katika mkutano uliofanyika jana mjini hapa.  

…………………………………………….

Na Lucas Raphael,Tabora

SERIKALI Mkoani Tabora imeomba Machifu kwa kushirikiana na Wazee wa Kimila na Viongozi wa madhehebu ya dini kufanya kile linalowezekana ili kudhibiti matukio ya mauaji yanayoendelea kujitokeza katika maeneo mbalimbali.

Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian alipokuwa akiongea na viongozi kutoka wilaya zote 7 za Mkoa huo na wadau wa maendeleo wakiwemo Watumishi wa Mungu na Machifu.  

Alisema matukio hayo yamekuwa yakiongezeka kila kukicha jambo ambalo halileti picha nzuri miongoni mwa jamii, hivyo akaomba Machifu na Wazee wa Kimila kulifanyika kazi ili kuepusha vitendo hivyo kwa watu wasio na hatia.

Aidha aliomba Maaskofu, Wachungaji, Mapadre na Mashekhe kutumia nyumba za ibada kukemea tabia hizo ili jamii iwe na hofu ya Mungu katika maisha yao na kuishi kwa amani na utulivu.

‘Hili la mauaji linamsononesha sana hata Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, linamkosesha usingizi, naomba sana ushirikiano wenu ili kukomesha vitendo hivyo’, alisema.

Balozi Dkt Batilda   alibainisha kuwa matukio ya namna hiyo yanaharibu sifa nzuri ya Mkoa huo hivyo akaomba Machifu, Viongozi wa Kimila, Wazee na sungusungu kutumia mbinu mbadala ikiwemo mikutano ili kudhibiti matukio hayo.

Kwa upande wake Chifu Kimwaga Msabila Lugusha wa Nguru ya Sikonge alisema kuwa wako tayari kulifanyia kazi huku akibainisha chanzo kikubwa cha mauaji hayo kuwa ni msukumo wa imani za kishirikina.

Alibainisha kinachotakiwa kuwa ni kuwakutanisha Machifu na Wazee wa kimila ili wafanye matambiko maalumu, ila maandalizi yanapaswa kufanyika kabla ya kufanya chochote, kuna vitu vinapaswa kununuliwa, wakivipata hamna shida.

Alitaja baadhi ya mahitaji kwa ajili ya kufanya shughuli hiyo kuwa ni ng’ombe, mbuzi, kondoo na vinginevyo, huku akibainisha manufaa mengine ya matambiko kuwa ni kukomesha vitendo vya wizi wa mali ya umma (ubadhirifu).

About the author

mzalendoeditor