Wahandisi wa TARURA wilayani Nzega Mkoani Tabora wakikagua moja ya barabara za vijijini zilizojengwa mwaka huu ili kurahisisha usafiri na usafishaji mazao ya wananchi.  

…………………………………………………………

Na Lucas Raphael,Tabora.

WATENDAJI wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoani Tabora wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea fedha za kutosha ili kufanikisha utekelezaji miradi ya barabara Vijijini na Mijini. 

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti walieleza kuwa Rais amesikia kilio cha wananchi, kwani Watendaji walikuwa wanashindwa kumaliza kero za ubovu wa barabara kutokana na ufinyu wa bajeti, sasa fedha zipo.

Walisema kuwa halmashauri zote za Mkoa huo sasa zina wakandarasi wanaoendelea na ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara za kiwango cha lami, changarawe na za udongo ambazo zilikuwa hazipitiki na sasa zinachongwa upya.

Waliongeza kuwa katika maeneo mengi ujenzi wa mifereji, makaravati na madaraja unaendelea kwa kasi kubwa na fedha za kuwalipa zipo, tofauti na hali ilivyokuwa huko nyuma.

Meneja wa TARURA wilayani Sikonge Mhandisi Eligidius Kaselwa alisema kuwa baada ya kuongezewa fedha za bajeti kutoka sh mil 889 hadi sh bil 4.19 matarajio yao ni kufungua mtandao mkubwa wa barabara wa zaidi ya km 1680.

‘Rais ametuheshimisha, tulikuwa tunasemwa vibaya na madiwani kwa kutotengeneza barabara zao, tulikosa raha kutokana na ufinyu wa bajeti, lakini sasa fedha zipo shida yetu ni magari, tuliyonayo yamechoka’, alisema.

Aidha alibainisha kuwa ili kuboresha zaidi utendaji wa TARURA aliomba Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuwajengea Ofisi za kudumu tofauti na hali ilivyo sasa ambapo wameazimwa Ofisi za taasisi nyingine.  

 Ofisa wa TARURA wilayani Nzega Mhandisi Mwera Makunge alisema kuwa baada ya kuwezeshwa na serikali sasa wanaweza kutengeneza mtandao mkubwa wa barabara kwa wakati mmoja tofauti na zamani, ila hawana magari ya kutosha.

Naye Mhandisi Simbuko Kyamba kutoka Nzega alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa Wakala huo sasa linaonekana baada ya kupewa bajeti za kutosha, ila akaomba mchakato wa usajili wa barabara upunguzwe ili kutochelesha maendeleo ya wananchi.

Meneja wa TARURA wilayani Kaliua Mhandisi Robert Kisandu aliishukuru serikali kwa kuwaongezea bajeti ya utekelezaji miradi ya barabara kiasi cha sh bil 5.9 katika mwaka wa fedha 2022/2023, huku akiomba serikali kuendelea kuwaongezea kila mwaka ili kumaliza kero zote.

Aidha kutokana na ukubwa wa mtandao wa barabara zitakazotengenezwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini aliomba serikali kuwaongezea magari ili kurahisisha ufuatiliaji miradi yote inayotekelezwa .

Previous articleSERIKALI YAWAANGUKIA MACHIFU,WAZEE WA KIMILA KUHUSU MAUAJI
Next article‘WATANZANIA WENGI WANATUMIA TIBA ASILI KUJITIBU’-DKT.CAROLINE DAMIANI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here