Featured Kitaifa

BINTI WA MIAKA 13 AUAWA KWA KUKATWA MAPANGA MOROGORO

Written by mzalendoeditor

Morogoro.

 Mwanafunzi wa darasa la saba shule ya msingi Mwenge iliyopo kata ya Kingolwira Manispaa ya Morogoro, Faidhat Ibrahimu (13) ameuawa kwa kukatwa mapanga na kaka yake.

Tukio hilo lilitokea Februari 15, 2022 usiku ambapo mtuhumiwa wa mauaji hayo anadaiwa kutoweka.

Akizungumzia tukio hilo leo mkuu wa upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Morogoro, Alpha Meela amesema chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi wa mirathi pamoja na imani za kishirikina.

“Kutokana na maelezo ya awali kwa watu ambao tumewahoji wanadai kuwa mtuhumiwa anatatizo la ukosefu wa nguvu za kiume na hivyo alikuwa akimtumuhu mama yake mdogo (mama wa marehemu) kuwa ndio amemloga,” amesema Meela.

Ameongeza kuwa binti huyo alikatwa mapanga wakati akiwa jikoni anaandaa chakula cha usiku na alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Morogoro.

Amesema kuwa baada ya kutokea kwa tukio hilo polisi walifika katika eneo la tukio ambapo mama mzazi wa mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi lakini pia kwa usalama wake kutokana na jamii kukasirishishwa na tukio hilo.

About the author

mzalendoeditor