Featured Michezo

”TTA SHIRIKIANENI NA SERIKALI KUKUZA MCHEZO WA TENIS’-YAKUBU

Written by mzalendoeditor

Adeladius Makwega-WUSM.

Serikali imevitaka vyama vya michezo nchini kushirikiana kwa karibu na serikali ili kufanikisha ukuaji wa michezo nchini.

Kauli hiyo imetolewa Februari 16, 2022 Mtumba jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Utamaduni Sanaa na Michezo Saidi Othman Yakubu wakati akizungumza na Rais wa Chama Cha Mchezo wa Tenisi Tanzania ndugu Denis Makoi.

“Sisi tupo tayari na tunashirikiana vizuri na mashirikisho, vyama vyote vya michezo nchini, na tunawakaribisha sana kwa ajili ya kushirikikana ili ushindi wa timu zetu ya Tenisi upatikane ndani na katika mashindano ya kimataifa.

Ameongeza kuwa, Viongozi wa wizara hiyo wameweka utaratibu wa kuzungumza na wadau wote wa sekta na tayari wamekutana na BMT, huku akiahidi kukutana na wadau hao.

Ndugu Yakubu amepongeza chama hicho, kwa kutekeleza vizuri shabaha ya mchezo huo, kwani timu za mchezo huo tayari zimefuzu kushiriki katika mashindano kadhaa ya kimataifa.

“Jukumu letu sisi ni kuhakikisha timu zetu za taifa za michezo yote zilizofuzu zinashiriki mashindano yote ya kimataifa kwa gharama za serikali, jukumu la wachezaji wetu ni kucheza kwa bidii, moyo na uzalendo ili kuleta ushindi kwa taifa letu.” amesisitiza Ndugu Yakubu

Awali Rais wa TTA nchini ndugu Makoi amesema kuwa anaishukuru serikali kwa kuwapa mwongozi mzuri wa kukiongoza chama cha mchezo huo ambao umetoa mwanga mpya kwa mchezo wa Tenisi nchini.
.
“Changamoto zetu zote nimeziwasilisha kwa serikali, ikiwemo la uhaba wa pesa na hilo serikali imetuhakikishia kulitatua kupitia bajeti ya wizara na wadau wengine wa michezo nchini.” amesema Ndugu Makoi.

About the author

mzalendoeditor