Featured Kitaifa

REA YAWASHA UMEME KWENYE ZAHANATI NA SHULE YA MSINGI MKOANI SIMIYU

Written by Alex Sonna

 

 

Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa mara ya kwanza, hivi karibuni wamewasha umeme katika Shule ya Msingi Nyangaka pamoja na Zahanati ya Nyakanga iliyopo katka Halmashauri ya wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu; tukio hilo limepokelewa kwa furaha na Walimu; Wanafunzi pamoja na Wananchi wanaoishi karibu na Kituo hicho cha Afya.

Mwalimu Mkuu wa Shula ya Msingi Nyangaka; Bi. Theresia Chuwa ameishukuru REA kwa kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika shuleni hapo na kuongeza kuwa utaboresha ufundishaji kwa kuwa hapo kabla masomo kadhaa yalikuwa yakifundishwa kwa nadharia zaidi si kwa vitendo.

“Shule yetu ilijengwa na kukamilika mwaka jana (2024) na hatukuwa na umeme, tuwashukuru sana REA kwani, imeturahisishia kwenye suala la ufundishaji, kwa sababu ya ukosefu wa umeme, sasa tunaweza kutumia vifaa vingi vya ufundishaji kwa vitendo kwa Wanafunzi”. Amesema Mwalimu Theresia.

Naye Muuguzi wa Zahanati ya Nyakanga, Bi. Maryciana Masanja ameishukuru Serikali kupitia REA kwa kupata umeme wa hakika na kuongeza kuwa, utawasidia katika utoaji wa huduma bora kwa Wananchi wa eneo hilo.

“Umeme utatusaidia kuhifadhi chanjo kwenye hali nzuri katika jokofu, pia tutakuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa nyakati zote hata katika wakati wa dharura, tutakuwa na uwezo wa kupokea mgonjwa wakati wowote”. Amesema Bi. Maryciana.

Wakati huo huo, Watumishi wa REA wamelishiriki katika zoezi la kuwasha umeme katika nyuma ya mwananchi mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Bibi Sophia Machumba anayeishi katika kijiji cha Mbiti, Halmashauri ya wilaya ya Bariadi.

Bi. Sophia amesema atautumia umeme kujiletea maendeleo pamoja na kuutimia kwa shughuli za kawaida ikiwemo ya uhakika wa mawasiliano kila atakapohitaji kuwasiliana na ndugu zake.

“Hapo kabla sikuwa na umeme, nilikuwa nikipeleka simu yangu mahali pengine kwa ajili ya kucharge na kuna nyakati simu ilikuwa ikipotea ila kwa sasa nitakuwa nikichaji simu yangu hapa hapa nyumbani kwangu”. Amesema Bibi Sophia.

About the author

Alex Sonna