Featured Kitaifa

SERIKALI YAAGIZA SEKRETARIETI YA AJIRA KUANZA MCHAKATO WA AJIRA MPYA

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Katika kuhakikisha changamoto ya uhaba wa watumishi wa umma inatatuliwa, Serikali imeielekeza Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuanza mchakato wa kujaza nafasi za upungufu wa watumishi katika taasisi mbalimbali kwa mwaka 2025/26.

Hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi katika utumishi wa umma, kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

Maelekezo hayo yametolewa leo Oktoba 11,2025 Jijini Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Juma Mkomi wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa kukamilishwa kwa mchakato wa ajira zote za mwaka 2024/25 ili kuhakikisha utoaji wa huduma kwa wananchi hauathiriki kutokana na uhaba wa rasilimali watu.

“Katika mwaka wa fedha 2025/26 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliidhinishwa nafasi 41,500 za ajira mpya kwa Taasisi mbalimbali zikiwemo nafasi 12,176 za Walimu na nafasi 10,280 za kada za Afya ambapo utekelezaji wake unaanza mara moja,”amesema.

Ili kupunguza gharama kwa waombaji, kuongeza uwazi wa mchakato wa ajira, pamoja na kuharakisha upatikanaji wa watumishi wenye sifa
Mkomi amewataka waajiri kutoa ushirikiano na waombaji kupata fursa ya kufanya usaili katika maeneo yao bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

“Ili kuhakikisha Sekretarieti ya Ajira inatekeleza jukumu hili ipasavyo, Waajiri wote wanaelekezwa kutoa ushirikiano, aidha, ninapenda pia kutoa maelekezo kwa Waajiri ambao Sekretarieti ya Ajira imekasimu madaraka ya uendeshaji wa mchakato wa ajira kwa baadhi ya kada, kuhakikisha wanaendesha usaili huu mara moja ili kujaza nafasi walizoidhinishiwa kwa kuzingatia Sheria, taratibu na Kanuni za uendeshaji wa usaili katika Utumishi wa Umma,”amesema.

Amesema kwa lengo la kuhakikisha zoezi la usaili linapunguza gharama na linafanyika kwa wakati, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imeelekezwa zoezi la usaili lifanyike kila Mkoa Tanzania Bara na vituo vilivyoandaliwa mahsusi kwa upande wa Zanzibar ili kutoa fursa kwa waombaji kutoka katika maeneo husika kuomba na hatimaye kusailiwa.

“Waombaji watakaofaulu usaili lakini wakashindwa kupangiwa kazi baada ya usaili wawekwe katika Kanzidata na waendelee kupangiwa kazi kwa kadri nafasi za ajira mpya zitakapokuwa zinapatikana, waombaji hawa watapangiwa kazi katika Taasisi zitakazokuwa na nafasi popote hapa nchini,”amesema.

Ameongeza kuwa barua za kupangiwa vituo vya kazi kwa wasailiwa watakaofualu usaili zipatikane katika “Mfumo wa Ajira Portal” kupitia akaunti za wahusika ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wake.

About the author

mzalendo