Spika wa Bunge la Ivory Coast, Amadou Soumahoro, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 68, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rais Alassane Ouattara.
Bw Soumahoro aliyefariki Jumamosi alikuwa mwanasiasa wa Ivory Coast na mfuasi mwaminifu wa Rais wa Ouattara. Alikuwa mwanachama mwanzilishi wa Rassemblement des Républicains (RDR), chama cha kihistoria cha Bw. Ouattara, mwaka wa 1994.
Waziri wa zamani wa biashara wa Ivory Coast, Amadou Soumahoro alikua spika ama rais wa Bunge la Kitaifa mwaka wa 2019, akichukua nafasi ya Waziri Mkuu wa zamani na kiongozi wa waasi Guillaume Soro.
Masuala ya kiafya yalimfanya awe nje ya nchi kwa muda mrefu katika miezi ya hivi karibuni. Mwaka jana, nafasi yake ilijazwa kwa muda na mmoja wa Makamu wa Rais wa Bunge la Kitaifa, Bw Adama Bictogo.