Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Yusuph Masauni mwaka 2018 akikagua ujenzi wa kituo cha polisi Ikungi wakati huo akiwa Naibu Waziri wa wizara hiyo,jengo hilo limetengewa kiasi cha Sh.Bil 1.1 ili kulikamilisha,pamoja nae ni mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Edward Mpogolo.
Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Yusuph Masauni akikagua kituo cha polisi Ikungi mwaka 2018 akiwa Naibu Waziri wa wizara hiyo,mbele yake ni mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu.
…………………………………………………..
SERIKALI kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema katika bajeti ya 2022/2023 ,imetenga kiasi cha Sh Bilioni 1.1 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa kituo cha polisi katika wilaya ya Ikungi Mkoani Singida.
Hatua hiyo imefuatia ombi alilolitoa Mbunge wa Singida Mashariki wakati akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2022/2023.
Akijibu hoja hiyo Mei 5,2022,bungeni Jijini Dodoma Waziri wa Wizara hiyo Mhandisi Hamad Yusuph Masauni amempongeza mbunge Mtaturu kwa kuwasemea askari.
“Nimpongeze Mtaturu kwa kuwasemea na kuwapambania askari wetu ili waweze kufanya kazi katika mazingira mazuri,nimhakikishie Mh Mtaturu kuwa katika bajeti hii tumetenga Sh.Bil 1.1 kwa hiyo ile bajeti yake ya Sh.Mil 600 kuna masalia yatabakia ,”alisema Masauni.
Katika mchango wake Mtaturu ameomba mambo matatu kwa Wizara hiyo ikiwemo kituo cha Polisi katika wilaya ya Ikungi na kuahidi kushika Shilingi endapo hatopata jibu la kuridhisha kuhusu ombi hilo.
Akichangia mjadala huo Mtaturu amesema kituo cha polisi kilichopo Ikungi kimeanza ujenzi katika miaka saba iliyopita.
“Kituo cha polisi kilichopo Ikungi kimeanza ujenzi miaka saba iliyopita,na ndani ya bunge hili nimeuliza maswali sio chini ya mara ya matatu kuhusu kituo kile na majibu yamekuwa ni yale yale,kwenye kituo cha polisi kinachotumika sasa hivi mnaweza kuseka ni stoo, sio kituo cha polisi chenye hadhi ya jeshi la polisi ,
Nimeona hapa imetajwa ndani ya bajeti na Mh Masauni tuliongea na wewe umeshafika pale 2018 ukiwa Naibu Waziri ,nikuombe sana kama sitopata majibu yakutosheleza kwa hakika kwa mara ya kwanza nitashika shilingi ili nipate ufafanuzi wa kutosha juu ya kituo cha Ikungi lakini na vituo vingine nchini, nini mkakati wa serikali katika kuhakikisha vituo hivyo vinajengwa na kuweka hadhi ya jeshi la polisi ambalo linafanya kazi vizuri sana,”alisisitiza.