Featured Kitaifa

MPANGO WA DAMU SALAMA WATAKIWA KUONGEZA USIMAMIZI UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA

Written by mzalendoeditor

Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali Dkt Saitole Laizer akizungumza Mkoani Morogoro katika hafla fupi ya kukabidhi vyeti vya Ithibati kwa vituo sita vya kanda za Mpango wa Taifa wa Damu Salama na Mpango wa Taifa wa Damu salama Zanzibar 5/5/2022

Washiriki wa hafla hiyo

Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali Dkt Saitole Laizer akimkabidhi cheti cha ithibati kwa mmoja wa wawakilishi wa Kanda za Mpango wa Taifa za Mpango wa Taifa wa Damu Salama katika hafla fupi ya kukabidhi vyeti vya Ithibati kwa vituo sita vya kanda za Mpango wa Taifa wa Damu Salama na Mpango wa Taifa wa Damu salama Zanzibar 5/5/2022 leo mkoani Morogoro.

Wawakirishi wa Kanda za mpango wa taifa wa damu salama wakiwa katika picha ya pamoja na meza kuu leo Mkoani Morogoro katika hafla fupi ya kukabidhi vyeti vya Ithibati kwa vituo sita vya kanda za Mpango wa Taifa wa Damu Salama na Mpango wa Taifa wa Damu salama Zanzibar.

Picha na Majid Abdulkarim WFA

……………………………………………………..

Na. WAF – Morogoro

Mpango wa Taifa wa Damu Salama nchini umetakiwa kuongeza juhudi katika kusimamia na kuratibu kazi zote zinazofanywa katika vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya Mikoa na halmashauri katika viwango vinavyokusudiwa ili viweze kupata utambuzi rasmi.

Hayo yamebainishwa na Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Saitole Laizer Mkoani Morogoro katika hafla fupi ya kukabidhi vyeti vya Ithibati kwa vituo sita vya kanda za Mpango wa Taifa wa Damu Salama na Mpango wa Taifa wa Damu salama Zanzibar ambapo amesema kuwa Tanzania inakuwa nchi ya tatu kupata Ithibati ya hatua ya tatu ya kuwa na vituo sita vya damu salama nchini vyenye utambuzi rasmi.

“Tanzania inaweza kuruhusiwa kuuza mazao ya Damu Salama mahali popote duniani kwani tumefikia viwango vya ubora vinavyokubalika kimataifa”, amesema Dkt Laizer.

Dkt. Laizer amesema chombo kinachotoa idhibati hiyo ni chombo cha kimataifa kinachoitwa Afrika Association of Blood Transfusion ambapo taasisi hiyo inapita kila nchi na kutizama ubora wa huduma ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama.

Dkt.Laizer metoa wito kwa Mpango wa Taifa wa Damu Salama nchini kuendelea kuhakikisha kwamba ubora wa Huduma uliopatikana katika hali ya juu bila kuteteleka.

“Maana kufikia kiwango cha juu ni hatua moja lakini kuendelea kubaki kiwango cha juu pia ni hatua nyingine”, amesema Dkt.Laizer

Dkt. Laizer amesisitiza Mpango wa Taifa wa Damu Salama Nchini kutatua changamoto zilizopo kuhakikisha wanalinda ubora walioupata na kwamba serikali iko bega kwa bega na kuona Mpango huo unakwenda kuwa endelevu na kuboreka kila mwaka.

Vituo sita vilivyopata ithibati hiyo ni Kanda ya Kaskazini Mkoa wa Kilimanjaro, Kanda ya Ziwa- Mwanza, Kanda ya nyanda za Juu Kusini- Mbeya, Kanda ya Magharibi- Tabora, Kanda ya Kusini- Mtwara pamoja na Mpango wa Taifa wa Damu Salama Zanzibar.

Akizungumza Dkt. Laizer amesema kuwa Mpango wa Taifa wa Damu Salama una jukumu kubwa la kuhakikisha unaelimisha, kuhamasisha, kukusanya damu kutoka kwa wachangiaji wa hiari na kusambaza katika vituo vya kutolea huduma nchini.

“Baada ya kukusanya damu hiyo huwa inachuguzwa kwa kupima magonjwa yote kabla ya kumhudumia muhitaji wa damu katika kituo husika”, ameeleza Dkt. Laizer

Kwa upande wake Mtekenolojia wa Maabara kutoka TAMISEMI Peter Torokaa amesema kuwa ili kufikia lengo la taifa ka kukusanya Damu chupa Laki tano na Hamsini Elfu kila mkoa unatakiwa kuchangia asilimia moja.

Naye, Mkurugenzi wa Tiba kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Amour Mohamed amesema kuwa hali ya upatikanaji damu salama ni nzuri ambapo lengo ni damu kumsubiri mgonjwa na sio Mgonjwa kusubiri damu.

Hata hivyo Meneja wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Dkt. Magdalena Lyimo amesema kuwa hali ya upatikanaji wa damu salama nchini ni asilimia 60 ambapo wanakidhi mahitaji ya nchi kwa sasa.

“Tunahitaji chupa 550, 000 kila mwaka ambapo kwa sasa tunakusanya chupa 330,000 kwa mwaka sawa na asilimia 60 ya mahitaji yetu”. amesema Dkt. Lyimo.

 

Vile vile Mkurugenzi Mwendeshaji wa MDH, Dkt. Nzove Ulenga amesema kuwa umoja na ushirikiano uloimarishwa baina ya MDH na Serikali kupitia Wizara ya Afya na Mpango wa Taifa wa Damu salama ndio chachu ya kupatikana kwa idhibati hizi zilizotolewa leo.

About the author

mzalendoeditor