MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian ,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 15,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025.
MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian ,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 15,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025.
SEHEMU ya Waandishi wa habari wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian (hayupo pichani) wakati akizungumzia Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025.
Na Alex Sonna-DODOMA
Mkoa wa Tanga umepokea zaidi ya shilingi bilioni 429.1 kwa ajili ya maboresho ya Bandari ya Tanga, ikiwa ni sehemu ya mikakati mikubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kubadilisha taswira ya mkoa huo kuwa kitovu cha biashara, usafirishaji, ajira na utalii wa kisasa katika Ukanda wa Kaskazini-Mashariki mwa Tanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian,ameeleza hayo Jana Jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani humo kwa kipindi cha miaka mitano (2020–2025) ikiwa ni utaratibu wa Idara ya Habari maelezo kutoa nafasi kwa wakuu wa mikoa kuzungumzia maendeleo kwenye maeneo Yao.
Amesema Bandari ya Tanga sasa inahudumia meli zaidi ya 307 kwa mwaka, ikilinganishwa na meli 198 zilizohudumiwa mwaka 2021. Aidha, shehena ya mizigo imeongezeka kutoka tani 888,130 hadi tani 1,191,480, ikiwa ni mafanikio makubwa yaliyochochewa na maboresho ya kimkakati ya miundombinu.
Dkt. Batilda pia amesema kuwa mafanikio ya bandari hiyo yameenda sambamba na ongezeko la fursa za ajira, ongezeko la mapato kwa mamlaka ya bandari, na kuvutia wawekezaji wa sekta binafsi ambao kwa sasa wanawekeza kwenye maghala, maeneo ya kuhifadhia mizigo na huduma za usafiri.
Pamoja na uwekezaji huo mkubwa,ameeleza kuwa Mkoa wa Tanga pia ni mwenyeji wa mradi mkubwa wa kimataifa wa bomba la mafuta ghafi (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga. Mradi huo ambao umefikia asilimia 53 ya utekelezaji, unahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilomita 205.91, kambi za wafanyakazi, vituo vya kuhifadhia mafuta, na mitambo ya usimamizi wa mradi.
Katika hatua za kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu kwenye utekelezaji wa mradi huo, Mkuu wa Mkoa amesema Serikali imelipa fidia kwa zaidi ya asilimia 98.7 ya wananchi waliopisha mkuza wa bomba.
Amefafanua kuwa Kati ya wananchi 1,580, jumla ya 1,560 tayari wamelipwa fidia yenye jumla ya shilingi bilioni 9.38, huku wengine 40 wakijengewa nyumba 43 mbadala ambazo tayari zimekamilika kwa asilimia 100.
Aidha, kupitia mradi huo, amesema zaidi ya ajira 810 zimezalishwa katika eneo la Chongoleani pekee, huku shughuli za kiuchumi kama vile mama lishe, huduma za usafiri, bidhaa ndogondogo na huduma za kifedha zikiongezeka kwa kasi kubwa.
Kwa upande wa sekta ya michezo, ameeleza kuwa Mkoa wa Tanga umepokea zaidi ya shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Michezo cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kinachojengwa eneo la Mnyanjani. Mradi huo unalenga kukuza vipaji vya vijana wa mkoa huo na kutengeneza fursa zaidi za ajira kupitia michezo na burudani.
Kwa upande mwingine, amesema Mkoa huo umewekeza katika miradi ya kibiashara kama vile ujenzi wa jengo la kisasa la Dkt. Samia Suluhu Hassan Business Centre, pamoja na soko la machinga la kisasa, miradi inayolenga kuhamasisha biashara ndogo na kati na kuongeza mapato ya Halmashauri.
Ameongeza kuwa kupitia mpango wa TASAF, zaidi ya walengwa 38,952 wameweza kuanzisha biashara ndogondogo, huku 48,645 wakijiunga na Bima ya Afya (CHF) na 44,234 wakijishughulisha na shughuli za kilimo na ufugaji. Amesema mafanikio haya yamekuwa nguzo ya ustawi wa familia nyingi vijijini na mijini.
Katika kuimarisha usafiri wa majini,Mkuu huyo wa Mkoa wa Tanga amesema Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya ukarabati wa kivuko cha MV Tanga, ambacho ni kiunganishi muhimu kwa wakazi wa maeneo ya mwambao. Huduma hiyo imeboreshwa ili kurahisisha usafirishaji wa abiria na bidhaa kati ya Tanga, visiwa vya jirani na maeneo ya pwani.
Amesisitiza kuwa Serikali pia imewekeza katika kuimarisha utawala bora kwa kujenga ofisi za utawala, nyumba za wakurugenzi, pamoja na kuongeza idadi ya mahakama za mwanzo kutoka 65 hadi 67, huku wilaya zikiongezeka kutoka 6 hadi 8, hatua inayolenga kusogeza huduma karibu na wananchi.