OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa maelekezo matatu kwa Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Wakuu wa vitengo vya Manunuzi kwenye Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia takwa la kisheria la kutumia mfumo wa kielektroniki wa ununuzi (NeST) na miradi inaendana na thamani ya fedha.
Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Festo Dugange ameyasema hayo leo Februari 4, 2025 jijini Dodoma alipokuwa akifungua kikao kazi kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na matumizi ya mfumo huo kwa niaba ya Waziri Mchengerwa, kilichohudhuriwa na Wabunge, Wakurugenzi na Wakuu wa vitengo vya manunuzi toka kwenye Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Katika hotuba yake, amesema amesema Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) inapaswa kusimamia sheria kwa kuhakikisha Taasisi nunuzi zote
zinafanya ununuzi kwa kutumia NeST.
“Chukueni hatua kwa wanaokiuka takwa hili la kisheria, kwani iko wazi hatua za kuchukua juu ya ukiukwaji wa utaratibu huu. Naelekeza kuhakikisha miradi yote inakuwa na thamani ya fedha na inakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa,”amesema.
Aidha, ameelekeza kuzingatia takwa la kutenga bajeti ya ununuzi kwa makundi maalum kama inavyoelekezwa na sheria.
“Nawaelekeza kusimamia fedha nyingi ambazo serikali imetenga na kuleta katika maeneo yenu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, nasisitiza hapa Mkurugenzi kushindwa kutekeleza moradi kwa wakati inawanyima haki wananchi kutumia miradi hiyo, hili halikubaliki kila mmoja atimize wajibu wake,”amesema.