Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akizungumza jambo wakati wa hafla ya kuitambulisha Kampuni ya ITHUBA kama mwendeshaji wa Bahati Nasibu ya Taifa baada ya kuibuka mshindi katika mchakato wa zabuni ulioendeshwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), katika Hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam, ambapo alisema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika michezo ya kubahatisha nchini kwa kuwa ni moja ya chanzo muhimu cha mapato ya kusaidia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Na. Joseph Mahumi, WF, Dar es Salaam
Serikali imeahidi kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika michezo ya kubahatisha nchini kwa kuwa ni moja ya chanzo muhimu cha mapato ya kusaidia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati wa hafla ya kutambulisha Kampuni ya ITHUBA kama mwendeshaji wa Bahati Nasibu ya Taifa baada ya kuibuka mshindi katika mchakato wa zabuni ulioendeshwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT).
Mhe. Chande alisema kuwa, Serikali inajivunia hatua ilizochukua kufanikisha mradi huo mkubwa wa mabadiliko ya Bahati Nasibu ya Taifa ambayo ni ishara ya matumaini, fursa na maendeleo, ambapo kila tiketi ya Bahati Nasibu inayonunuliwa, mbali na nafasi ya kushinda, ni mchango kwa maendeleo ya Taifa letu.
Aliongeza kuwa uteuzi wa Kampuni ya ITHUBA Tanzania kama mwendeshaji rasmi wa Bahati Nasibu ya Taifa unaonesha uwezo wao wa hali ya juu na uelewa wa kina wa mahitaji ya Tanzania na uteuzi huo ulizingatia utaalam na uzoefu wa ITHUBA, kama mwekezaji wa kimataifa mwenye rekodi nzuri ya kuendesha biashara ya Bahati Nasibu za Taifa barani Afrika ambako inaendesha michezo hiyo katika nchi ya Afrika ya Kusini, Uganda na nyinginezo.
“Ni imani yangu kuwa ITHUBA imejipanga vyema ili Bahati Nasibu ya Taifa iweze kuendeshwa kwa ufanisi na kuleta mafanikio yaliyotarajiwa na hatua hii inafungua matarajio makubwa katika ufanisi wa uendeshaji wa Bahati Nasibu ya Taifa na ukurasa mpya wa mabadiliko katika sekta ya michezo ya kubahatisha hapa nchini Tanzania” alisema Mhe. Chande.
Aliongeza kuwa katika nchi mbalimbali duniani, Michezo ya Bahati Nasibu ya Taifa imeonesha uwezo wa kuleta mabadiliko makubwa kwa kuzalisha mapato ya kusaidia vipaumbele vya kitaifa, na hapa Tanzania, Bahati Nasibu ya Taifa itafuata mkondo huo huo kwa kuhakikisha kuwa mapato yake yanatumika moja kwa moja kwa manufaa ya taifa, huku ikizingatia viwango vya juu vya uwazi, uwajibikaji, na uadilifu chini ya usimamizi madhubuti wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT).
Mhe. Chande alitoa wito kwa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), kuhakikisha wanatekeleza matakwa ya Sheria inayosimamia michezo hiyo katika uendeshaji wake na kuhakikisha Bahati Nasibu ya Taifa inakidhi matarajio ya kuanzishwa kwake kwa kuleta manufaa kwa wananchi wa Tanzania.
“Bahati Nasibu ya Taifa ni zaidi ya mchezo wa kubahatisha, kwani ni fursa muhimu ya uwezeshaji wa kiuchumi na maendeleo ya jamii ikiwemo kukuza vipaji vya michezo na kama ilivyobainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya GBT, Mhe. Balozi Modest Mero, asilimia hamsini (50%) ya mapato yatakayokusanywa kupitia kodi za mchezo huu, yataelekezwa katika kukuza na kufadhili shughuli za maendeleo ya michezo nchini na Ushirikiano huu unashikilia maono ya pamoja yanayounganisha Serikali, waendeshaji, na washiriki katika kujenga mustakabali bora kwa wote” alisema Mhe Chande.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya GBT, Mhe. Balozi Modest Mero, alisema kuwa bodi ya wakurugenzi wa GBT, imeridhishwa na rekodi thabiti na uzoefu wa kampuni ya ITHUBA katika tasnia hiyo hasa katika uendeshaji wa Bahati Nasibu za Taifa katika nchi mbalimbali barana Afrika na wanaimani ni mshirika bora katika kuendesha Bahati Nasibu hapa Nchini.
“Kampuni hii imeonyesha uwezo na utayari wa kuleta Bahati Nasibu ya Taifa ambayo tulikuwa tunaikusudia na kuisubiria na hivyo sisi kama bodi tunashukuru sana ushirikiano na uungawaji mkono wa Serikali katika mradi huu kupitia Wizara ya Fedha” alisema Mhe. Balozi Mero.
Kampuni ya ITHUBA itaendesha Bahati Nasibu ya Taifa kwa muda wa miaka nane (8), ambapo watawekeza zaidi ya dola za kimarekani milioni 20 katika biashara hiyo, ambayo italeta fursa mbalimbali za maendeleo na kukuza ajira endelevu zitakazoimarisha uchumi na kuinua jamii.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akizungumza jambo wakati wa hafla ya kuitambulisha Kampuni ya ITHUBA kama mwendeshaji wa Bahati Nasibu ya Taifa baada ya kuibuka mshindi katika mchakato wa zabuni ulioendeshwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), katika Hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam, ambapo alisema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika michezo ya kubahatisha nchini kwa kuwa ni moja ya chanzo muhimu cha mapato ya kusaidia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) (Kulia), akiteta jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania GBT, Mhe. Balozi Modest Mero wakati wa hafla ya kuitambulisha Kampuni ya ITHUBA kama mwendeshaji wa Bahati Nasibu ya Taifa baada ya kuibuka mshindi katika mchakato wa zabuni ulioendeshwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), katika Hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam, ambapo Katika hafla hiyo Mhe. Chande alisema kuwa, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika michezo ya kubahatisha nchini kwa kuwa ni moja ya chanzo muhimu cha mapato ya kusaidia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) (Katikati), Mwenyekiti wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania GBT, Mhe. Balozi Modest Mero (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Bw. James Mbalwe (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi wa Kampuni ya ITHUBA Tanzania, Bw. Kelvin Koka (wa pili kulia), na Mkuu wa Masoko na Masuala ya Kampuni wa ITHUBA Afrika, Bi. Michelle Van Trotsenburg (wa kwanza kulia), wakifuatilia maswali ya wanahabari wakati wa hafla ya kutambulisha Kampuni ya ITHUBA kama mwendeshaji wa Bahati Nasibu ya Taifa baada ya kuibuka mshindi katika mchakato wa zabuni ulioendeshwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) (Katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania GBT, Mhe. Balozi Modest Mero (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Bw. James Mbalwe (wa pili kulia), Mkurugenzi wa Kampuni ya Ithuba Tanzania, Bw. Kelvin Koka (wa kwanza kushoto), na Meneja wa Masoko wa Kampuni ya Ithuba Afrika, Bw. Mpange Chapeshamano, kabla ya kufanyika kwa hafla ya kuitambulisha Kampuni ya ITHUBA kama mwendeshaji wa Bahati Nasibu ya Taifa baada ya kuibuka mshindi katika mchakato wa zabuni ulioendeshwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) (Katikati mstari wa mbele), Mwenyekiti wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania GBT, Mhe. Balozi Modest Mero (wa nne kushoto), Mkurugenzi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Bw. James Mbalwe (wa tatu kushoto), Mkurugenzi wa Kampuni ya ITHUBA Tanzania, Bw. Kelvin Koka (wa nne kulia), Mkuu wa Masoko na Masuala ya Kampuni wa ITHUBA Afrika, Bi. Michelle Van Trotsenburg (wa tatu), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Wizara ya Fedha, Bodi ya GBT na Kampuni ya ITHUBA, baada ya kumalizika kwa hafla ya kuitambulisha Kampuni ya ITHUBA kama mwendeshaji wa Bahati Nasibu ya Taifa baada ya kuibuka mshindi katika mchakato wa zabuni ulioendeshwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), katika Hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)