*Na WMA – Mwanza*
Banda la Wakala wa Vipimo (WMA) limeendelea kuvutia makundi mbalimbali ya wananchi katika Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayoendelea katika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, ikiwa ni siku ya tatu, Agosti 30, 2026.
Makundi hayo yameonesha kuvutiwa na elimu ya vipimo tofauti tofauti.
Wakiwa bandani hapo, wengi wa wanafunzi na vijana wameonesha kuvutiwa zaidi na elimu ya matumizi ya mizani za kielektroniki na pampu za kupimia mafuta.
Wamesema elimu hiyo inawapa uelewa wa kuwa mabalozi wa vipimo shuleni na majumbani mwao huku wengine wakidai ndoto yao ni kuwa Maafisa Vipimo wa baadae.
Kwa upande wa akina mama wajasiriamali, wengi wamejikita kujifunza kuhusu matumizi sahihi ya mizani inayotumika masokoni na waliuliza maswali mengi kuhusu namna ya kutambua ujazo wa mtungi wa gesi ya kupikia wanapoenda kununua.
Wengi wameipongeza WMA kwa kuwaelimisha jinsi ya kuepuka hasara na kuhakikisha mteja anapata haki yake.
Askari na wazee waliotembelea Banda la WMA wameonesha kuvutiwa na elimu ya vipimo katika sekta ya mafuta ya petroli, saruji na bidhaa nyingine za ujenzi. Askari wamesema elimu hiyo itawasaidia katika doria za kuhakikisha biashara inafanyika kwa haki, wakati wazee wamesema wamepata uelewa mpya wa kulinda familia zao dhidi ya udanganyifu.
Wananchi wote waliotembelea banda hilo wamepongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kuwa na Wakala wa Vipimo nchini. Wamesema uwepo wa WMA umesaidia kulinda haki za walaji na kuweka mazingira bora ya biashara yanayosadifu kaulimbiu ya maonesho isemayo “Usalama na Amani ni Kichocheo cha Biashara na Uwekezaji”.
