Featured Kitaifa

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YANOLEWA

Written by mzalendo

Na Mwandishi wetu- Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imelipongeza Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake ipasavyo kuhakikisha kunakuwa na ushiriki wa Wananchi katika shughuli za uchumi na kujiletea maendeleo.

Pongezi hizo zimetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Florent Kyombo wakati wa semina ya kuijengea uwezo kamati hiyo iliyotolewa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kuhusu majukumu yake, muundo wake na namna inavyofanya kazi zake kuwafikia wananchi katika ukumbi wa Bunge, jijini Dodoma.

Mhe. Kyombo alisema utolewaji wa elimu hiyo umesaidia kuwaongezea uelewa kuhusu baraza hilo na namna linavyowahudumia wananchi akisema ni hatua nzuri kuelekea maboresho ya muswada unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni.

“Kamati imepokea elimu hii nzuri, wote tumeelewa vizuri na hii imetupa mwanga naamini itasaidia katika maboresho ya huu muswada ulioko mbele yetu,” alipongezw Mhe. Kyombo.

Awali akizungumzia majukumu ya baraza hilo Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi. Beng’I Issa amesema miongoni mwa kazi zake ni pamoja na Kuratibu shughuli za uwezeshaji nchini, kuonesha na kutoa fursa za ushiriki wa watanzania kiuchumi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na kuwaunganisha watanzania na fursa hizo.

“Kazi zingine tunazofanya kama baraza ni kuandaa Mikakati, Miongozo na programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Kuwezesha vikundi, biashara za ndani na ubia katika shughuli za kiuchumi kwa kushirikiana na wadau, kuishauri serikali, sekta za umma, sekta binafsi kuhusu kuendeleza uwezeshaji kiuchumi Tanzania,” alisema Katibu Mtendaji huyo.

Aliendelea kufafanua kwamba Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lilianzishwa mnamo 2004 likifanya kazi zake chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa mujibu wa sheria namba 16 iliyopitishwa na Bunge mwaka 2004 kikiwa ni chombo cha juu cha kutoa uongozi kwa ajili ya Uwezeshaji wa kiuchumi.

“Baraza hili lina dhamana ya kupanga, kuratibu, kuwezesha, kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambapo utekelezaji wake unafanywa na sekta zote,” alieleza.

Sambamba na hilo Katibu Mtendaji huyo alibainisha kwamba ili kuwafikia wananchi kwa urahisi katika maeneo yao, Serikali iliamua kuanzisha Vituo Maalum vya kuhudumia wananchi kwenye masuala yote ya kiuchumi walengwa wakiwa ni wajasiriamali wote wakiwemo wadogo, wakati na wakubwa, vikindi na makampuni yaliyopo katika sekta zote za kiuchumi.

“Uanzishwaji wa kituo cha uwezeshaji ni utaratibu muafaka ambao utaondoa adha ya watanzania katika kutafuta taarifa, elimu na ujuzi kwenye maeneo ya biashara na mambo mengine ya kiuchumi, kufahamu taratibu za urasimishaji wa biashara, taarifa za masoko, kuongeza thamani ya mazao, kufahamu fursa za hifadhi ya jamii, kupata elimu ya kodi na kufahamu fursa za mitaji.

Hata hivyo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga alieleza kwamba Serikali itaendelea kuboresha miundo mbinu wezeshi itakayowasaidia wananchi kufanya shughuli zao vizuri kwa kuzingatia ukuaji wa teknolojia na kujongezea kipato.

About the author

mzalendo