Featured Kitaifa

NAIBU WAZIRI MKUU BITEKO AIPONGEZA WIZARA YA MADINI KWA MPANGO WA KUONGEZA AKIBA YA DHAHABU NCHINI

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Bombambili, Geita.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko ameipongeza Wizara ya Madini kwa mkakati wanaoutekeleza ambao unawazesha upatikanaji wa akiba ya Dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania jambo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya Uchumi wa Tanzania.

Hayo yamesemwa jana Oktoba 05 2024 wakati wa ufunguzi wa maonesho ya saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yenye kauli mbiu ya “Matumizi ya Teknolojia sahihi ya Nishati safi katika sekta ya Madini kwa maendeleo endelevu” yanayofanyika Mkoani Geita.

“Sisi utajiri ambao Mungu ametujalia ni utajiri wa madini ikiwemo Dhahabu, lazima madini haya yawe chachu katika ukuaji wa uchumi wetu.

Naipongeza Wizara ya Madini kwa bidii kubwa mlioifanya sasa ya kuanzisha na kusukuma uwepo wa akiba ya Dhahabu kupitia Benki kuu ya Tanzania”, alisema Mhe. Biteko.

Kwa upande wake Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameeleza kwamba kwa sasa baada ya kukaa pamoja baina ya serikali na wadau wamefikia muafaka na hakuna mgomo tena wa kutoiuzia Dhahabu BOT baada ya ufafanuzi wa baadhi ya hoja na elimu kutolewa ikiwa ni sehemu ya falsafa ya maridhiano inayohubiriwa kwa nguvu na Mhe. Rais Dkt. Samia S. Hassan.

Mhe. Mavunde ametoa rai kwa wadau wote kushirikiana na serikali katika mpango huu wa upatikanaji wa akiba ya dhahabu kupitia BOT na kuahidi kutoa ushirikiano katika kushughulikia changamoto mbalimbali zitakazojitokeza.

Akitoa maelezo ya awali, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za kukuza Sekta ya Madini hasa kwa Wachimbaji wadogo na kuahidi kwamba Mkoa wa Geita utaendelea kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya madini ambapo mkoa huo ni mzalishaji mkubwa wa madini ya dhahabu.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Kilumbe Shabani Ng’enda ameeleza kuwa Kamati inaridhishwa na mwenendo wa Wizara ya madini hususan inavyosimamia sheria na sera ya madini kwa manufaa ya uchumi wa watu na nchi kwa ujumla.

Akitoa salamu zake, Rais wa Shirikisho la Vyama cha Wachimbaji Madini(FEMATA) Ndg. John W. Bina ameipongeza Wizara ya Madini kwa usikivu na majadiliano ya mara kwa mara pindi changamoto zinapojitokeza na kuahidi kwamba baada ya kikao cha pamoja wadau wameridhia mpango wa serikali wa ununuzi wa dhahabu kupitia BOT.

About the author

mzalendo