Featured Kitaifa

WANAFUNZI WALIOATHIRIKA NA VITA YA UKRAINE WAPATIWA USHAURI WA KISAIKOLOJIA

Written by mzalendoeditor

Wahadhiri wa ISW ambao pia ni wataalam wa saikolojia wametoa huduma ya ushauri wa kisaikolojia kwa wanafunzi wa kitanzania waliokuwa wanasoma Ukraine mwishon mwa Juma katika ukumbi wa Chuo kikuu Huria Tanzania.

Huduma hiyo imetolewa katika mkutano maalum uliowakutanisha na uongozi wa Wizara ya Elimu, Mwenyekiti wa kamati ya wazazi wa wanafunzi wanaosoma vyuo vya nje ya nchi ,Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Global Education Link na wataalamu wa saikolojia kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii iliyo chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum.

Wakiongea katika mkutano huo wazazi wa wanafunzi hao ambao waliambatana nao katika mkutano huo wameelezea jinsi ambavyo watoto wao hawapo katika hali ya kawaida kutokana na athari ya vita, hali ya kukatishwa masomo ghafla wengi wao imewafadhaisha sana, na baadhi wamekata tamaa ya kuendelea kusoma kwa kutokujua hatima yao ya kimasomo, wapo ambao hawatoki ndani na hawana hamu ya kula walisema.

Akitoa elimu hiyo mtaalamu wa saikolojia kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii Richard Haule aliwashauri wanafunzi hao kujiepusha kuangalia habari au taarifa zozote za vita ili kusahau waliyopitia pindi wapo Ukraine na kujitahidi kufanya shughuli nyingine kama michezo,shughuli za kijamii ili kusahau masuala ya vita. Kujitahidi kujisomea mambo mengine ya kimasomo na ya kijamii ya kawaida ili kutoa msongo wa mawazo walio nao kwa sasa.

“Wazazi, huu sio muda wa kulaumiana na watoto bali ni muda wa kutulia kimawazo ili kutafuta namna bora ya kutumia fursa zinazokuja za kimasomo na maisha kwaajili ya watoto wenu, ili kuona njia bora ya kutimiza ndoto zao ambazo lazima ziendelee bila ya kukatishwa tamaa na janga la vita. Wazazi msikate tamaa kuendelea kuwagharamia masomo watoto wenu” alisema msaikolojia Haule.

Kwa upande wa wanafunzi, wameshukuru sana elimu na ushauri wa kimawazo waliopata kutoka kwa wanasaikolojia na kusema imesaidia sana kwasababu hawakuwa sawa na elimu hii imewapa mwanga na matumaini mapya.

“Baada ya vita kuanza, nilikuwa katika hali ya kukataa kama kweli kuna vita na ninatakiwa kuondoka, ( i was in a state of denial) nilimwambia baba yangu sirudi Tanzania vita itaisha tuu, kumbe sikuwa sawa mpaka Mama alipoongea na mimi sana na kukubali kurudi nyumbani.” Alisema Franco Macho Mwanafunzi wa udaktari wa tiba za binadamu na upasuaji mwaka wa pili aliyekuwa akisoma sumy state university nchini Ukraine.

About the author

mzalendoeditor