Featured Kitaifa

RC MKIRIKITI:“WAKUU WA WILAYA MSICHEKE NA WAHARIBIFU WA MAZINGIRA”

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akifungua kikoa cha tathmini ya utunzaji mazingira kwa wadau wa mkoa huo jana mjini Sumbawanga ambapo ameagiza wakuu wa wilaya kuchukua hatua kwa wote wanaokiuka sheria za utunzaji mazingira.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Rukwa Daniel Ntera amesema taasisi yake itaendelea kuchukua hatua kali za kuwakamata watendaji wote wa umma wanaoshindwa kusimamia sheria za utunzaji misitu na mazingira.

Mtendaji wa taasisi ya REYO Bw. Issa Rubega  ameshauri wadau wa mazingira kutoa ufadhili kwa wananchi wanaofanya kazi za uzalishaji miche ya miti ili wasambaze kwa wingi kwa jamii hatua itakayowezesha uhifadhi wa mazingira.

Mshauri wa Maliasili Mkoa wa Rukwa Nicholaus Mchome akitoa taarifa kuhusu hali ya uharibifu wa mazingira na mzisitu kwa mkoa wa Rukwa ambapo katika mwaka 2018/2019 jumla ya hekta 45,530 za misitu kati ya hekta 190,870 ziliungua moto.

 Wadau wa misitu na mazingira wakiwa kwenye kikao cha tathmini jana mjini Sumbawanga ambapo mkakati umewekwa wa kuondoa watu wote wanaoishi na kufanya shughuli katika misitu ya hifadhi na vyanzo vya maji kote mkoani Rukwa.

Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijuakali ameshauri watumishi wa TFS  kuhakikisha vibali vinavyotolewa kwa ajili ya uvunaji mazao ya misitu vinatumika katika maeneo yaliyokusudiwa ili kulinda maliasili za taifa.
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa)

…………………………………………..

Na. OMM Rukwa

Wakuu wa Wilaya za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo katika mkoa wa Rukwa wametakiwa kuchukua hatua za haraka kudhibiti wananchi wanaoharibu mazingira kupitia shughuli za kibinadamu ikiwemo uchomaji moto na kilimo kwenye maeneo ya vyanzo vya maji.

Akifungua kikao cha tathmini ya utunzaji mazingira na usimamizi endelevu wa maliasili jana (08 Aprili, 2022) mjini Sumbawanga, Mkuu wa Mkoa huo Joseph Mkirikiti alionya dhidi ya kuongezeka kasi ya uharibifu wa misitu na maeneo ya vyanzo vya maji.

“ Wakuu wa wilaya msicheke na wanaoharibu mazingira yetu, chukueni hatua kwa watu wote wanaoharibu Misitu kwa kutumia sheria zilizopo ili tunusuru misitu ya mkoa wa Rukwa na vyanzo vya maji ambavyo vinateketea kila siku kutokana na watu wachache wasiotaka kutii sheria” alisema Mkirikiti.

Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kusema wananchi wasipoelimishwa vya kutosha juu ya sheria za uhifadhi wa mazingira kuna hatari kubwa siku za usoni Misitu na vyanzo vya maji vikamalizika na kusababisha janga kwa maisha ya vizazi vijavyo.

Mkirikiti akizungumzia takwimu za misitu alisema mkoa wa Rukwa una hekta 190,870 za Misitu ambapo katika mwaka 2018/2019 jumla ya hekta 45,530 ziliungua kwa moto kutokana na shughuli za kijamii.

“Maeneo yote ya Misitu ya hifadhi na vyanzo vya maji tusiruhusu watu waishi au kufanya shughuli za kibinadamu kwani ni kinyume cha sheria na pia ni utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais Dkt. Phillip Mpango” alisisitiza Mkirikiti.

Aidha alieleza athari za uharibifu wa mazingira kuwa ni pamoja na  uvamizi wa vyanzo vya maji mto Lwiche,uvamizi wa shughuli za kibinadamu katika msitu wa hifadha Kalambo hatua inayoweza kuathiri uwepo wa maporomoko ya Maji Kalambo ambayo ni kivutio cha utalii.

Kwa upande wake Mshauri wa Maliasili mkoa wa Rukwa Nicholaus Mchome alisema kutokuzingatiwa na kusimamiwa kwa sheria ya mazingira namba 20 ya mwaka 2004 na sheria ya Misitu namba 14 ya mwaka 2002 ndio chanzo kikbwa cha uharibifu unaonekana katika mkoa wa Rukwa.

Mchome aliongeza kusema changamoto iliyoukabili mkoa huo ni wananchi wengi kutegemea rasilimali za Misitu kwa ajili ya nishati ya mkaa na kuni majumbani.

Naye Mhifadhi Wilaya ya Sumbawanga toka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Herman Ndazi alisema sababu kuu zinazopelekea uharibifu wa mazingira ni pamoja na kilimo cha kuhama hama, idadi kubwa ya Mifugo ,uanzishwaji holela wa makazi na uwindaji wa panya unaopelekea uchomaji moto.

Ndazi alitaja madhara yalioyanza kuonekana mkoa wa Rukwa ni pamoja na  vyanzo  maji kukauka, kutoweka kwa viumbe hai na kina cha ziwa Rukwa kupungua kutokana na kujaa tope.

Kwa upande wake Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Rukwa Daniel Ntera alishauri watendaji wa serikali na viongozi kuzingatia sheria za uhifadhi ikiwemo utoaji wa vibali vya kuvuna na kusafirisha mazao ya Misitu uwe wazi  .

Ntera aliwataka watumishi wa umma kusimamia sheria ili hifadhi ya mazingira na Misitu iendelee kuwa tija kwa taifa na kuwa eneo hilo TAKUKURU inaendelea kudhibiti mianya ya rushwa.

“Sisi tukigundua kuna sheria haijasimamiwa na TFS tunachukua hatua za kufuatilia kwani kutosimamia sheria ni ishara ya uwepo wa mianya ya rushwa hivyo tutakuja na kuwakamata tujue kwanini rasilimali za misitu zikiteketea “alisisitiza Ntera.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wadau wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, wahifadhi wa Misitu, wadau wa mazingira wakiwemo LEAT, TFS, KAESO, SUWASA, RUWASA, na wajumbe wa Kamati ya Usalama Mkoa.

About the author

mzalendoeditor