Wananchi wamesisitizwa kutumia Nishati Safi ya Kupikia na kuachana na Nishati isiyo kuwa salama ili kulinda afya zao, kutunza mazingira pamoja na kuondokana na athari za kijamii na kiuchumi zinazotokana na matumizi ya kuni na mkaa.
Kauli hiyo imetolewa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson wakati wa hitimisho la Tamasha la mashindano ya mapishi ya vyakula kwa kutumia Nishati safi ya kupikia ( Tulia Cooking Festival) lililofanyika Agosti 31, 2024 jijini Mbeya.
“Lengo la kuandaa Tamasha hili ni kuongeza uhamasishaji kwa jamii kuhusu elimu na matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na wote tunafahamu kwamba ajenda hii imebebwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa Nishati Safi ya Kupikia Afrika na sasa ametambuliwa pia duniani kwa ujumla.” Amesema Dkt. Tulia
Ameeleza kuwa tamasha hilo limehusisha Mamalishe na Babalishe 1,000 ambapo amewapongeza kwa kutumia Jukwaa hilo ili kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na kuzitaka taasisi mbalimbali nchini kuandaa matamasha kama hayo ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Aidha, amewapongeza wadau wa maendeleo kwa kudhamini Tamasha la Tulia Cooking Festival ikiwemo Kampuni ya gesi ya ORYX, Cocacola, EWURA na wadau wengine ambao wamewezesha elimu ya Nishati Safi ya Kupikia kufikia wananchi wengi zaidi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali imeandaa Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia ili kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati hiyo ifakapo mwaka 2034.
“Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kuhamasisha Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa kutoa mitungi ya gesi ambapo mwaka 2023 Serikali ilitoa zaidi ya mitungi 104,000 na mwaka huu inategemea kutoa mitungi 450,000.” Amesema Kapinga.
Ameongeza kuwa, nishati safi za kupikia zipo za aina nyingi ikiwemo gesi, umeme, majiko banifu na majiko mengine, pia amesisitiza kuwa nishati safi ni bora kwa kuandaa chakula kuliko nishati nyingine kama kuni na mkaa.
Kuhusu kupunguza bei ya gesi, amesema Serikali inaendelea na mikakati ya kuwasaidia watu wengi waweze kutumia nishati hiyo kwa gharama nafuu na amezitaka kampuni za gesi kuendelea kufanya ubunifu ili kuhakikisha wananchi wananunua gesi kwa kiasi cha fedha walichonacho.