Featured Kitaifa

SERIKALI KUJENGA BARABARA YA MASASI – LIWALE KM 175 KWA AWAMU

Written by mzalendo

Serikali imesema inaendelea na utaratibu wa ujenzi wa barabara ya Masasi –Nachingwea- Liwale yenye urefu wa KM 175 kwa awamu ili kuendelea kurahisisha shughuli za kiuchumi na biashara kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Maimuna Ahmad Pathan alietaka kujua ni lini Serikali itaijenga barabara ya Masasi- kwenda Liwale kupitia Nachingwea kwa kiwango cha lami.

“Mhe. Spika naomba nimhakikishie Mhe. Mbunge kwamba taratibu za ujenzi wa barabara hiyo zinafanyika kwa awamu kutokana na upatikanaji wa fedha”, amesema Naibu Waziri Kasekenya.

Katika hatua nyingine, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi Milioni 500 kwa ajili ya usanifu na matengenezo ya barabara zilizoathiriwa na mvua katika kipindi cha mwaka 2024 – 2025 ikiwemo barabara ya Kongowe –Mjimwema  Bhadi Kivukoni KM 25.   

Naibu waziri Kasekenya alikuwa akijibu swali la Mbunge Viti Maalum Mariam Kisangi alietaka kujua ni lini Serikali itakarabati barabara ya Kongowe-Mjimwema iliyoathiriwa na mvua za El- Nino.

About the author

mzalendo