Na. James K. Mwanamyoto OR-TAMISEMI
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Mhe. Zainab Katimba amewataka wasimamizi wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa shule za Sekondari maalum 26 za wasichana za mikoa, kuhakikisha wanasimamia vizuri matumizi ya fedha zilizotolewa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kujenga shule hizo ili ziwe na viwango bora vitakavyowawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri.
Mhe. Katimba ametoa maelekezo hayo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa, alipoitembelea Shule Maalum ya Wasichana ya Mkoa wa Kigoma kwa lengo la kujiridhisha na kiwango cha ujenzi wa shule hiyo ambayo imejengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza.
“Nimeridhishwa na kiwango cha ujenzi wa shule hii Maalum ya Wasichana ya Mkoa wa Kigoma ambayo ilipokea fedha za Mhe. Rais Samia kiasi cha shilingi bilioni 3 katika awamu ya kwanza awamu ya kwanza shilingi bilioni 3 na awamu ya pili itapelekwa bilioni 1.1,” Mhe. Katimba ameeleza.
Aidha, Mhe. Katimba ametoa wito kwa Wakurugenzi wengine wa Halmashauri nchini wanaosimamia Ujenzi wa Shule za Sekondari Maalum za Wasichana katika mikoa mingine, kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya kuendeleza miundombinu hiyo ya shule iliyojengwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuunga mkono jitihada zake.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais, na ni wazi kuwa anafanya jitihada za makusudi ambazo zinazoonekana na ushaidi ni hii shule Maalum ya Wasichana ya Mkoa wa Kigoma yenye maabara, mabwalo, mabweni, madarasa na nyumba za walimu zenye viwango bora kabisa,” Mhe. Katimba amesisitiza.
Kwa upande wake Bw. Khamis Rajabu ambaye ni Mkazi wa Uvinza mkoani Kigoma amemshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa shule hiyo ya wasichana mkoani kigoma, ambayo imetatua changamoto iliyokuwa ikiwakabili ya watoto wa kike kukosa shule ya sekondari yenye viwango bora.
Naye, Odetha Denis ambaye ni Mwanafunzi wa Shule Maalum ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Kigoma, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua thamani ya watoto wa kike na kuwajengea shule hiyo itakayowawezesha kusoma na kufikia ndoto zao kama ilivyo kwa watoto wa kiume.
Mwanafunzi mwingine wa shule hiyo, Amina Albano amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea shule yenye miundombinu bora iliyowawezesha watoto wa kike kutoka katika maeneo mbalimbali nchini kupata shule nzuri itakayowarahishia kufikia malengo yao kitaaluma.
Shule hii mpya ya Wasichana ya Mkoa wa Kigoma ina vyumba vya madarasa 12, maabara 4, jengo la utawala, matundu ya vyoo 16, bwalo la chakula, nyumba za walimu 2, mabweni 8, jengo la wagonjwa, chumba cha Jenereta, kichomea taka, matanki ya ardhini ya kutunzia maji 2, matanki ya plastiki ya maji 2 na matanki ya maji Taka 2.