Vicky Kimaro na Mwanahamisi Msangi, Dodoma.
SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imepiga marufuku Halmashauri kutoza tozo kwa Wachimbaji ambazo zipo kinyume na Sheria mama huku kliniki ya kutibu changamoto za wachimbaji wa madini ikipangwa kuanza Julai 3 2024, nchi nzima.
Akizungumza leo Juni 26, 2024 katika Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), Naibu Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, amesema tozo yoyote inayoangukia kwenye Sekta ya Madini ni lazima ioane na Sheria mama.
“Ni marufuku na hili ni agizo kwa halmashauri zote nchi nzima, kutoza tozo ambazo ni kinyume na sheria mama, tozo zote zioane na haziwezi kuwa juu ya sheria mama, ili sheria iweze kuwasaidia wachimba madini ni lazima ifanyiwe mapitio. “Sisi kupitia maelekezo ya mama yetu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alishaelekeza sheria na Wizara zote kuhakikisha zinasomana, tupo kwenye mchakato na wenzetu wa TAMISEMI kuzipitia, kubainisha sheria zao na ‘bylaw’ zao ambazo zinaingilia sekta yetu, zinakwaza wawekezaji katika Sekta ya Madini,” amesema Dkt. Kiruswa.
Aidha, Mhe. Dkt. Kiruswa amesema Wizara itaanza kliniki kuanzia Julai 3, 2024 ya kusikiliza na kutatua changamoto za wadau wa Sekta ya Madini kwa kushirikiana na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, na kusema “Kliniki hii ni mahususi tukifika‘site’ changamoto ambazo Wizara tutaweza kuzitatua hapo kwa hapo tutafanya hivyo, za kisheria na kimifumo tutakwenda kushirikisha wadau husika.”amesisitiza Mhe. Dkt. Kiruswa.
Pia, amesema Wizara ipo kwenye mchakato wa kufanya marekebisho ya Kanuni mbalimbali za Sekta ya Madini na kueleza kwamba katika bajeti ijayo ya Mwaka wa Fedha 2024/25 kiasi kikubwa cha bajeti kimeelekezwa katika shughuli za utafiti huku tafiti hizo zikiwalenga wachimbaji wadogo ili wachimbe kwa tija.
“Tafiti zitatusaidia kujua madini tuliyonayo, aina tulizonazo, sehemu yalipo, ubora wake na pale tunapogawa zile leseni mtu anapoomba leseni hata iwe ndogo apewe leseni ambayo tayari taarifa za Stamico zipo,’’ amesema Mhe. Dkt. Kiruswa.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kiruswa ameiagiza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kutoa ripoti ya utafiti kwa umma na sio kuzifungia kwenye makabati.
Vilevile, Mhe. Dkt. Kiruswa amesema, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa wachimbaji na kutoa rai kwa wachimbaji kutoa ushirikiano katika maeneo matatu, ikiwemo kuendelea kuwa vinara wa kutii na kufuata Sheria ya Madini na Kanuni zake.
Sambamba na hilo, Mhe. Dkt. Kiruswa amewataka wachimbaji kuwa mabalozi wa mfano wa kufuata taratibu na kupambana na utoroshwaji wa madini na kuwataka kuzuia madini kutoroshwa kwa sababu yanavyotoroshwa yanalikosesha taifa mapato huku akiwataka kuendelea kuzitumia Taasisi za Wizara kutekeleza majukumu yao.
Wakati huo huo, Mhe. Dkt. Kiruswa amezielekeza Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa zote pale wanapokwenda kwenye shughuli zao au mikutano yao wasiende bila kuwa na wawakilishi wa wachimbaji (REMAs).
Kwa upande wake, Rais wa FEMATA John Bina, amewataka wachimbaji wadogo kuipa muda Serikali ili iweze kushughulikia changamoto zao ambazo wameziwasilisha ikiwa ni pamoja na kuishauri Serikali wanachokitaka kwa maslahi ya Taifa.
“Sisi kama Shirikisho tunaandaa makongamano na mikutano maana yake ni kuishauri Serikali na viongozi kwa sababu sisi ndio wenye sekta kwani huwezi kuwa mwanachama wa FEMATA kama siyo mchimbaji wa madini ili uwe na uchungu na kile unachozungumzia,” amesema Bina.
Mkutano wa FEMATA unakwenda sambamba na maonesho ya madini na vifaa vya uchimbaji pamoja na kongamano la wachimbaji.