Featured Kitaifa

WALEMAVU WA NGOZI JIEPUSHENI NA MAZINGIRA YANAYOWEZA KUHATARISHA AFYA ZENU – NDERIANANGA

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Serikali imetoa wito kwa Watu wenye Ualbino kutambua mahitaji na haki zao kiafya na kujiepusha na mazingira yanayoweza kuhatarisha afya zao.

Hayo yameelezwa leo Mei 27,2024 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga
wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Khadija Shaban Taya aliyetaka kujua ni lini Serikali itahakikisha kunakuwa na maeneo maalum kwa Watu wenye Ualbino kwenye mikutano ya hadhara ili wasikae juani.

“Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu 2004, kupitia matamko yake namba 3:11- Uondoaji Vikwazo vya Ufikivu, 3:1-Matunzo kwa Watu wenye Ulemavu, 3:13 -Marekebisho na 3:14-Mchangamano, imeonesha namna ambayo watu wenye Ulemavu wakiwemo wenye Ualbino wanavyostahili kushiriki na kushirikishwa katika shughuli za kijamii na kisiasa”,amesema.

Aidha, ameongeza kuwa Serikali kwa kuzingatia nyaraka hizio muhimu, inatoa wito kwa viongozi wote wa Serikali na Taasisi zake pamoja na wadau wa huduma za kijamii kuhakikisha kuwa wakati wa utoaji wa huduma, suala la ufikivu na usalama kwa Watu wenye Ualbino linazingatiwa.

About the author

mzalendo