Featured Kitaifa

MADAKTARI 1,109 KUNUFAIKA NA UFADHILI WA RAIS SAMIA KATIKA MASOMO YA UBINGWA BOBEZI 2023/24

Written by mzalendo

Na WAF – Dar Es Salaam

Dkt. Samia Super-Specialized scholarship Programme imetoa nafasi za ufadhili wa masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi ambapo kwa mwaka wa masomo 2023/2024, jumla ya Shilingi 10.9 bilioni zimetengwa na kuwawezesha wanafunzi 1,109 kwenye masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo Mei 2, 2024 wakati akifungua mkutano wa Mwaka wa chama cha Madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani Tanzania (APHYTA) uliofanyika katika ukumbi wa Kinataifa wa Mwalim Julius Nyerere Jijini Dar Es Salaam.

“Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa madaktari bingwa katika kuwaendeleza kitaaluma kupitia programu ambayo imetoa nafasi za ufadhili wa masomo ya ubingwa kwa mwaka wa Masomo 2023/2024, kwa wanafunzi 1,109 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 582 ukilinganisha na mwaka wa masomo 2022/2023.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, katika idadi ya wanafunzi wote ambao wamepata ufadhili kupitia programu hiyo, wanafunzi 79 watasomea udaktari bingwa wa magonjwa ya ndani na kati yao madaktari 11 sawa na asilimia 33 wamekwenda kusoma ubingwa bobezi wa magonjwa ya ndani.

Aidha, Waziri Ummy ametoa wito kwa madaktari vijana kujitokeza kwa wingi kwenda kujiendeleza katika masomo ya ubingwa bobezi hususan kwenye magonjwa ya ndani na wakirudi wakubali kupangiwa sehemu yoyote kwa kuwa Mikoa mingine pia inahitaji madaktari bingwa bozezi.

“Kupitia muundo huu mpya wa Sekta ya Afya, tutaweza kuwatambua kwa kuwawekea mazingira mazuri madaktari wenye Ubobezi katika maeneo mbalimbali ikiwemo wa masuala ya magonjwa ya ndani.” Amesema Waziri Ummy

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amewataka madaktari hao kujadiliana na kuja na mapendekezo ya jinsi ya kupunguza magonjwa Yasiyoambukiza kwa kuwa kwa sasa kumekuana ongezeko kubwa la magonjwa hayo.

Pia, Waziri Ummy amewataka madaktari hao kujadiliana na kutoa maoni yao katika muongozo wa Kitaifa wa matibabu pamoja na orodha ya Taifa ya dawa ili kama kuna mapungufu yaweze kurekebishwa.

“Suala la kitita cha Bima ya Afya NHIF linatakiwa lijadiliwe kuanzia kwenye muongozo wa Kitaifa wa matibabu pamoja na orodha ya Taifa ya dawa, tukishakuliana tunamwambia NHIF atambue na afuate mabadiliko hayo.” Amesema Waziri Ummy

About the author

mzalendo