Featured • Kitaifa

WAKALA WA VIPIMO MKURANGA WAFANYA UKAGUZI WA KUSHTUKIZA KWA WAUZAJI WA GESI YA KUPIKIA

Written by Alex Sonna

 

 

 _Na WMA – MKURANGA_ 

Wakala wa Vipimo (WMA) umekagua mizani na mitungi ya gesi ya kupikia inayouzwa kwa wananchi katika eneo la Vikindu Mkoani Pwani, na kubaini kuwa vipimo vilivyokaguliwa vinakidhi viwango vinavyotakiwa, hatua inayolenga kuwalinda walaji dhidi ya udanganyifu na hasara wakati wa kununua gesi kwa matumizi ya nyumbani.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Vipimo Mwandamizi wa WMA Mkoa wa Ki-vipimo Mkuranga, Tatu Samweli amesema katika ukaguzi huo wa kushtukiza, wamekagua mizani inayotumika kupimia gesi pamoja na mitungi ya uzito tofauti, ikiwemo ya kilo sita, kilo 14 na kilo 66, na kubaini kuwa vipimo hivyo vinakidhi viwango vinavyotakiwa.

Amesema wananchi wanapaswa kuhakikisha kuwa wanaponunua gesi, wanapata uzito unaolingana na ulioandikwa kwenye mtungi. Ameongeza kuwa ni muhimu kutumia mizani iliyokaguliwa na Wakala wa Vipimo ili kuepuka malalamiko ya kuishiwa gesi mapema kutokana na uwezekano wa kununua kiasi kisicholingana na kilicholipiwa.

Aidha, amewashauri wananchi kuangalia alama au stika ya WMA inayoonyesha kuwa mizani imekaguliwa na kuthibitishwa kuwa inafaa kutumika, ili kuhakikisha wanapata huduma na vipimo sahihi.

Kwa upande wake, Jonas Mzava, mfanyakazi wa Bright Vision, kampuni inayosambaza gesi kwa mawakala na wauzaji, amesema wanaunga mkono zoezi hilo kwa kuwa linaongeza imani ya wateja kwa wafanyabiashara na kuwasaidia wananchi kupata huduma inayozingatia usahihi wa vipimo.

Amesema ukaguzi huo pia unasaidia kupunguza sintofahamu zinazoweza kujitokeza katika biashara ya gesi, huku akiwataka wafanyabiashara wenzake kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo katika uuzaji na usambazaji wa mitungi ya gesi.

Naye Kaimu Mohamed, mkazi wa Bagamoyo, ameishukuru WMA kwa kufikisha huduma hiyo karibu na wananchi, akisema ukaguzi huo unasaidia kuhakikisha kuwa mtungi unaonunuliwa una uzito ulioainishwa, kwa mfano mtungi wa kilo sita unakuwa na uzito unaotakiwa.

Kwa upande wake, Rukia Mohamed, mkazi wa Dar es Salaam, amesema zoezi hilo lina umuhimu kwa watumiaji wa gesi majumbani kwa kuwa linasaidia kulinda maslahi yao na kupunguza uwezekano wa kuuziwa gesi isiyolingana na uzito ulioainishwa kwenye mtungi.

About the author

Alex Sonna