Mahakama ya Uchaguzi Nchini Afrika Kusini imeamua Rais wa zamani wa nchi hiyo Jacob Zuma kuwa anaweza kugombea katika uchaguzi kama mgombea wa Chama cha Umkhonto weSizwe (MK).
Siku ya jana mahakama hiyo ilitupilia mbali uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini (IEC) wa kumzuia Zuma kugombea kiti cha Bunge.
IEC ilisema hangeweza kuwa mgombea kwa sababu alihukumiwa kifungo cha miezi 15 kwa kudharau mahakama ila Mahakama imebatilisha uamuzi huo.
Mwishoni mwa mwezi Machi, Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini ilipitisha pingamizi dhidi ya rais wa zamani, Jacob Zuma, kugombea uchaguzi mkuu wa mwezi Mei, ikinukuu kipengele cha Katiba kinachosema mtu aliyehukumiwa kifungo cha miezi 12 au zaidi hawezi kuchaguliwa kwa miaka 5.
Hata hivyo, chama cha MK kimewasilisha ombi la kupinga kuenguliwa kwake kwenye kinyang’anyiro hicho cha uchaguzi, kikisema kuwa Zuma alitumikia miezi mitatu pekee kati ya miezi 15 aliyotakiwa kuhudumu kabla ya kusamehewa na agizo la Rais Cyril Ramaphosa.
Uchaguzi mkuu wa Afrika Kusini utafanyika Mei 29, wakati wananchi watakapopigia kura Bunge jipya la Kitaifa na mabunge ya majimbo.
Wafuasi wa chama cha MK walionya kuwa wataandamana na kuvuruga zoezi la kupiga kura iwapo wagombea wake hawataruhusiwa kugombea.
Aidha, Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini iliwataka raia kutokubali majaribio ya kuvuruga uchaguzi huo, ikionya kwamba wale wanaotishia utulivu katika uchaguzi huo watakabiliwa na hatua za kisheria.