Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Theopista Mallya amewataka waumini wa Dini ya kiisilamu kuhimiza watu kuacha kujihusisha na vitendo vya kikatili katika jamii zinazowazunguka huku akieleza baadhi ya Mambo yanayosababisha ukatili ikiwa ni pamoja na ulevi wa kupindukia na lugha chafu.
Ameyasema hayo Machi 29, 2024 alipokuwa akizungumza na waumini wa dini ya kiisilamu katika swala ya Ijumaa msikiti wa Gadafi na kusema kuwa ushirikina ni jambo ambalo linapelekea ukatili hasa watu wanapoenda kwa waganga kutafuta utajiri na kupewa masharti ambayo yatawafanyia watoto vitendo vya kikatili ambavyo ni kuwalawiti na kuwabaka ili wapate utajuri kwani hata vitabu vya dini vinakataza vitendo hivyo.
Kamanda Mallya amewataka wazazi kuwa karibu na watoto wao ili kujua Kama kuna changamoto wanazo kutananazo mashuleni, majumbani au hata njiani ili kuweza kubaini na kuzifanyia kazi kwani kumekuwepo na wimbi kubwa la mapenzi ya jinsia moja hasa kwa Vijana na nichukizo kwa mwenyezi Mungu na hata vitabu vitakatifu vya dini vimekataza.
Kwa upande wake shekhe Mkuu wa Mkoa Dodoma ambaye ndiye Imam wa Msikiti wa Gadafi Mustapha Rajabu Shabani amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kwa kazi kubwa na nzuri wanayoendelea kuifanya hasa katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani ambacho waumini wengi wapo katika mfungo ili watu watambue Haki na kujua batili ni Nini na vitendo vya ukatili kwani Viongozi wa kidini ni walinzi wa amani wa kiroho na Polisi ni walinzi wa kimwili.
Pia Sheikhe Mustafa amesema ieleweke kuwa hii elimu inayotolewa na Jeshi la Polisi ni ibada kwani kumsaidia au kumuelimisha mtu kuacha uhalifu ni kuacha kutenda dhambi.