Na. Asila Twaha, Tanga
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeutaka uongozi wa Mkoa wa Tanga kusimamia miradi ya maendeleo katika Halmashauri zote za Mkoa huo.
Wito huo umetolewa leo na Mhe. Ally Makoa (Mb) wakati akisoma majumuisho na pendekezo ya Kamati kwa uongozi wa Mkoa wa Tanga mara baada ya Kamati hiyo kuhitimisha ziara ya kikazi ya kukagua miradi inayotekelezwa katika Halmashauri za Wilaya ya Korogwe, Mji Korogwe, Muheza, Jiji la Tanga, Pangani na Mkinga mkoani Tanga.
Akieleza kutoridhishwa na matumizi ya fedha za umma zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Tanga, Mhe. Ally amesema mapungufu yaliyobainika yanatokana na usimamizi usioridhisha katika ngazi ya mkoa hivyo uongozi unapaswa kuhakikisha miradi inasimiwa ipasavyo.
Amesema, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga ina nafasi kubwa ya kuhakikisha Halmashauri zinatekeleza miradi yote kwa kuzingatia kanuni, sheria, taratibu na miongozo iliyopo ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria kwa watumishi watakaobainika kutumia vibaya fedha za miradi.
Pamoja na mapendekezo mengine Kamati imeitaka Ofisi ya Rais -TAMISEMI kuhakikisha inafanya uchunguzi wa kina juu ya matumzi ya shilingi bilioni 2.550 katika Hospitali ya Wilaya ya Mkinga ambazo zimetumika hatimaye kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria kwa watakaobainika kufanya matumizi mabaya ya fedha za umma.
Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais -TAMISEMI Dkt. Charles Msonde ameishukuru Kamati ya LAAC kwa kufanya ziara Mkoa wa Tanga na kuhaidi kusimamia maelekezo yote yaliyotolewa na kamati hiyo kwa maslahi ya umma.
Aidha, Dkt. Msonde ametoa wito kwa watumishi wa Halmashauri zote nchini kutekeleza miradi kwa mujibu wa Sheria,Kanuni na Taratibu zilizopo ili miradi ikamilike kwa wakati na kuwanufaisha wananchi.