Featured Kitaifa

WAKURUGENZI TAMISEMI NA WIZARA YA AFYA FUATILIENI KUJUA IDADI YA VIJIJI VISIVYO NA ZAHANATI – DKT MOLLEL

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewaomba Wakurugenzi wa TAMISEMI na Wizara ya Afya kuangalia idadi ya Vijiji ambavyo havina Zahanati ili kuweza kuhakikisha vinapata vituo hivyo.

Dtk. Mollel ametoa ombi hilo leo Machi 27,2024 wakati akifunga Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi uliofanyika Jijini Dodoma kwa muda wa siku Tatu ambapo washiriki mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi waneshiriki katika kuchangia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika mkutano huo.

“Tukijipanga kwa muda wa miaka miwili tukapunguza semina na makongamano na tukapunguza mengine na mengine, tukapunguza kidogo kuboresha huku juu zaidi kwasababu huku tunaweza kwenda kwa pamoja nawahakikishia kwa kipindi cha miaka miwili hakuna Kijiji kitakosa Zahanati,”amesema.

Amesema hiyo itasaidia watakapokutana tena katika mkutano kama huo mwaka 2026 kuzungumza masula mengine kama kuweka watumishi, kuweka vifaa na kuboresha huduma zingine zinazopaswa kuwekwa.

Aidha amewaomba washiriki katika mkutano huo kuwasaidia wakurugenzi ambao bado wanaleta mgawanyiko katika kazi kuhakikisha suala hilo wanalimaliza na kuimarisha utendaji zaidi.

“Sekta ya Afya ni moja na kazi nyingi za afya zinaanzia katika ngazi ya msingi na dada yangu Dkt. Grace amesisitiza hapa hakuna huduma za afya bila msingi kwani huduma zote zinaanzia huko na wananchi wengi ndipo wanaanzia kabla ya kuja huku juu kupatiwa huduma,”amesema.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Charles Mahela amesema kuwa kupitia mkutano huo mapendekezo mbalimbali yameweza kutolewa kupitia majadiliano yaliyofanyika ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kutosha kwa huduma za afya ya msingi.

“Mapendekezo hayo ni pamoja na kuongeza bajeti za afya za mifumo ya bima na jambo hili limesisitizwa kwa ukubwa na wakashauri vyanzo mbalimbali viweze kutumika ikiwemo kuwashirikisha wadau kama Wizara ya Fedha,”amesema.

Amesema pendekezo lingine lililotolewa ni kwa wadau pamoja na Serikali ni kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya afya ya msingi kwenye rasilimali watu na vifaa ili kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora.

About the author

mzalendo