Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais -TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amewataka watumishi wa Afya nchini kufanyakazi kwa weledi na miiko ya utumishi katika kutoa huduma kwa wananchi.
Dkt. Mfaume ametoa maelekezo wakati akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Nzega Mji ambapo amewataka watumishi hao kutumia kauli ambazo ni faraja kwa mgonjwa na wafanyakazi katika eneo la kutolea huduma.
“kuna wachache wetu ambao wanaharibu taswira ya watumishi wa Afya na bahati nzuri tunafahamiana ukiuliza kwenye hospitali hii wangapi wanalalamikiwa unakuta ni walewale wanalalamikiwa kwa kauli chafu kwa wagonjwa au watumishi wenzao”.Amesema Dkt. Rashid Mfaume
Akisisitiza hilo amesema hapendezwi na tabia za baadhi ya watumishi wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kuwarekodi wenzao na kusambaza mitandaoni ili watu waanze kutafsiri tabia zao jambo ambalo ni kinyume cha maadili.
“kuna tuhuma ambazo baadhi yenu mnapewa ukihusishwa na tabia fulani lakini unakuta sio kweli”Amesema
Timu wa Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI ikiongozwa na Mkurugenzi Dkt. Rashid Mfaume ipo mkoani Tabora kwa ziara ya kukagua miradi ya Afya na kufuatilia ufanisi na utendaji wa watoa huduma za Afya ngazi ya wilaya na mkoa.