Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale ameitaka timu ya uchambuzi wa Mipango na Bajeti ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuhakikisha kuwa inafanya kwa umakini mkubwa zoezi la Uchambuzi wa Bajeti za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa fedha 2024/2025 ambalo linaendelea kupitia mfumo wa PlanRep katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais -TAMISEMI Dodoma.
Bw. Mtwale ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma, wakati alipotembelea kujua hatua iliyofikiwa na Timu ya uchambuzi wa mipango na bajeti ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI ambayo hukaa kila mwaka kuchambua mipango na bajeti za Serikali za Mitaa kwa lengo la kuhakikisha Mipango hiyo imezingatia maelekezo na miongozo ya Serikali ili iweze kutekelezeka kwa ufanisi.
“Hakikisheni mnachambua vema mipango na bajeti iliyowasilishwa ili zilenge kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi,” Bw. Mtwale amesisitiza.
Sanjari na hilo, Bw. Mtwale ameitaka timu hiyo kuhakikisha halmashauri zote zinatenga fedha za kukamilisha miradi viporo yakiwemo maboma ili miradi hiyo ianze kutoa huduma kwa wananchi, kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi mipya kwa sekta husika.
Aidha, ameilekeza timu hiyo kupitia kwa umakini mipango ya halmashauri zote zinazopokea fedha za uwajibikaji wa makampuni (CSR) ili kuhakikisha fedha hizo zinalenga kutatua changamoto ambazo wananchi wamekuwa wakikabiliana nazo kila mara.
Bw. Mtwale amemalizia kwa kusisitiza kuwa zoezi hilo la uchambuzi wa mipango na bajeti ni muhimu katika kufikia vipaumbele vya kitaifa, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa hivyo linapaswa kutekelezwa kwa ufanisi.