Kimataifa

14 WAPOTEZA MAISHA KUSINI MWA NIGERIA KWA HOMA YA LASSA

Written by mzalendo

Panya ndio wasababishaji wakuu wa homa hatari ya Lassa

Mamlaka za afya ya umma nchini Nigeria zimetangaza kuwa, idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na homa ya Lassa katika jimbo la Ebonyi la kusini mwa nchi hiyo imeongezeka kutoka watu 10 hadi 14 tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2024.

Hyacinth Ebenyi, mkurugenzi wa afya ya umma wa jimbo la Ebonyi, amewaambia waandishi wa habari katika mamao makuu ya jimbo hilo yaani Abakaliki kwamba, watu 14 ni miongoni mwa wagonjwa waliothibitishwa kufariki dunia kwa homa ya Lassa kufikia sasa.

Kwa uchache kesi 110 zinazodhaniwa kuwa ni za homa ya Lassa zimesajiliwa huko Ebonyi tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2024.

Hyacinth Ebenyi amesema kuwa, kuna ongezeko kubwa la kesi za homa ya Lassa hivi sasa na ni janga katika jimbo hilo.

Homa ya Lassa ni ugonjwa unaoenea kwa wanadamu kupitia chakula au vitu vya nyumbani vilivyochafuliwa na mkojo wa panya au kinyesi. Inasemekana kuwa huwa unaambukizwa wakati mate, mkojo na kinyesi cha panya vinapogusana na wanadamu.

Mripuko wa hivi sasa ugonjwa wa huo huko Ebonyi umechochea kufanyika juhudi za haraka za ushirikiano kati ya serikali kuu na mamlaka husika kwa ajili ya kukomesha kueneakwa ugonjwa huo unaoambukizwa kwa kasi kubwa.

Serikali ya jimbo la Ebonyi ilisema Jumapili wiki hii kwamba kwa uchache watu 25, wakiwemo wafanyikazi wawili wa afya, waliambukizwa ugonjwa huo katitika kipindi cha baina ya Januari 4 hadi Februari 16.

Hyacinth Ebenyi amesema kwamba ugonjwa huo huambukizwa sana wakati wa kiangazi, akiwataka watu kuacha kula panya na wasiruhusu wadudu hao kugusa vyakula vyao.

Mwaka 2023, kwa uchache watu 219 walifariki dunia kati ya kesi 1,227 zilizothibitishwa za homa ya Lassa nchini Nigeria.

About the author

mzalendo