Featured Kitaifa

BODI YA EWURA YAZITAKA MAMLAKA ZA MAJI NCHINI KUTATHMINI HUDUMA ZAKE

Written by mzalendoeditor

 

Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Prof Mark Mwandosya( katikati) akizungumza jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa TUWASA Mha.Mayunga Kashilimu ( wa pili kulia) wakati Bodi hiyo ilipotembelea Mamlaka hiyo ya maji  . Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Tuwasa, Nick Mlimuka. Wengine katika picha ni watumishi wa TUWASA, EWURA na wajumbe wa Bodi ya EWURA.

Na.Mwandishi Wetu 

Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji( EWURA) imezielekeza Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini
kutathmini huduma kwa wateja wake ili kupata mrejesho utakaozisaidia kuboresha utendaji na huduma zao kwani suala hilo ndilo msingi wa utendaji bora.

Bodi hiyo, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Mark Mwandosya, imetoa maelekezo hayo  wakati wa ziara yake kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya mjini Tabora (TUWASA) kufuatilia utendaji wake na kujiridhisha juu ya utekelezaji wa maelekezo yanayotolewa na EWURA kwa mamlaka za maji nchini.

“Kwa niaba ya Bodi, napenda kuwakumbusha TUWASA na mamlaka zote za maji nchini kutathmini huduma zinazotolewa kwa wateja, fanyeni utafiti wa namna wateja wanavyoridhishwa na huduma zenu ili muweze kupima utendaji wenu” Alisisitiza.

Bodi ya EWURA pia, imezitaka mamlaka za maji kuweka utaratibu wa kukutana na wateja wao, kuwaelimisha mara kwa mara kuhusu haki na wajibu wao na kutatua changamoto zinazowakabili wateja ili kuleta tija na ufanisi wa utendaji.

Bodi ilipata wasaa wa kutembelea chanzo cha maji cha Bwawa la Igombe lenye lita za ujazo milioni 36, miundombinu ya matenki ya kupokelea maji kutoka Ziwa Victoria eneo la Itumba na kwenye matenki yaliyopo Kazehil yanayosambaza maji kwenye kata takribani 20 za mji wa Tabora.

Wengine walioshiriki ziara hiyo ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Bi. Victoria Elangwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Bodi ya Maji, Mha. Ngosi Mwihava, na mjumbe Bwana Haruna Masebu.

Mwenyekiti wa Bodi ya TUWASA, Bw. Dick Mlimuka ameihakikishia Bodi ya EWURA kuyatekeleza maelekezo yaliyotolewa ili kuendelea kuleta tija kwenye huduma za maji na usafi wa mazingira mjini Tabora.

Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Prof Mark Mwandosya( katikati) akizungumza jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa TUWASA Mha.Mayunga Kashilimu( wa pili kulia) wakati Bodi hiyo ilipotembelea Mamlaka hiyo ya maji  . Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Tuwasa, Nick Mlimuka. Wengine katika picha ni watumishi wa TUWASA, EWURA na wajumbe wa Bodi ya EWURA.

Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA , Prof Mark Mwandosya ( mwenye mkongojo) katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya TUWASA, Bw. Nick Mlimuka ( wa tatu kutoka kulia) wakurugenzi wa TUWASA na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Bi Victoria Elangwa(wa nne kutoka kushoto) katika chanzo cha maji cha Bwawa la Igombe, nje kidogo ya mji wa Tabora, wakati Bodi ya EWURA ilipofanya ziara ya kikazi kukagua miundombinu ya maji ya mamlaka ya maji TUWASA.

Wajumbe wa Bodi ya EWURA, kutoka kushoto Mha. Ngosi Mwihava, mwenyekiti Prof Mark Mwandosya, Makamu Mwenyekiti Ms Victoria Elangwa na kulia ni Bw. Haruna Masebu, wakiwa katika chanzo cha maji cha bwawa la Igombe mjini Tabora wakati Bodi hiyo ilipofanya ziara ya kikazi kufuatilia utendaji wa Mamlaka ya Maji Tabora.

Bodi ya na watendaji wa EWURA na ya TUWASA, wakiwa mbele ya chanzo cha maji cha bwawa la Igombe mjini Tabora wakati wa ziara ya kikazi kwenye miundombinu ya ya mamlaka ya maji Tabora kutathmini hali ya utoaji huduma za maji na usafi wa mazingira.

Wajumbe wa Bodi na Watendaji wa EWURA katika chanzo cha maji cha Bwawa la Igombe Tabora, wakati wa ziara ya Bodi ya EWURA kutathmini utendaji wa TUWASA.

Bodi ya EWURA, TUWASA na watendaji wakiwa katika tanki la maji la Kazehill wakati wa ziara ya kikazi ya Bodi ya EWURA.

Bodi ya EWURA na TUWASA na watendaji wao wakiwa katika eneo lilipo tenki la maji Itumba, linalopokea maji kutoka ziwa Victoria ili kusambaza kwa wateja mjini Tabora wakati wa ziara ya kukagua utendaji wa TUWASA.

 

About the author

mzalendoeditor