Na. WAF, DAR ES SALAAM
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Mwaka 2023 Tanzania iliweza kuvutia Wagonjwa 6,931 kutoka nje ya Nchi kufika nchini kwa ajili ya kupata huduma za matibabu katika Hospitali sita hapa nchini.
Waziri Ummy amebainisha hayo leo Januari 10, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar Es Salaam akiwasilisha taarifa ya hali ya utoaji huduma za afya nchini kwa mwaka 2023 na vipaumbele vya Sekya ya Afya Mwaka 2024.
Waziri Ummy amesema kwa mwaka 2022 idadi ya wagonjwa kutoka nje ya nchi waliofika nchini Tanzania kwa ajili ya matibabu ilikuwa ni 5,705 hivyo kufanya idadi hiyo kuongezeka kwa asilimia 121 hadi kufikia wagonjwa 6931 mwaka 2023.
Amebainisha kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kuboresha huduma za kibigwa na bobezi katika sekta ya afya umesaidia kuvutia nchi jirani kufata Huduma za afya nchini.
Waziri Ummy amesema kuwa Wagonjwa hao wanatoka katika Nchi za Comoro, Malawi, Burundi, Zambia, Congo DRC, Uganda, Zimbabwe na Kenya ambapo walihudumiwa katika Hospitali sita ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Taasisi ya Mifupa MOI, Hospitali ya Agha khan na Hospitali ya Saifee.