Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
MAMLAKA
ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Tanzania imepokea ujumbe kutoka
Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya nchini Burundi (CMA – Burundi)
unaojumuisha Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Timu ya
Wataalamu kwa ajili ya kufanya ziara ya mafunzo ya siku tano.
Ujumbe
huo utafanya ziara katika Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana
(CMSA), Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Kampuni za Usimamizi wa
uwekezaji na watendaji wengine katika masoko ya mitaji huku ikielezwa
ziara hiyo imelenga kujenga uelewa wa namna masoko ya mitaji
yanavyoendeshwa.
Pia kuainisha masuala muhimu yatakayoiwezesha
nchi ya Burundi kuwa na masoko ya mitaji imara, himilivu, yenye ufanisi
na yatayowezesha kuwa na matokeo chanya katika kuchochea ukuaji wa sekta
ya fedha na uchumi nchini Burundi kama ilivyo nchini Tanzania.
Akizungumza
leo Desemba 20, 2023 jijini Dar es Salaam Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA
CPA. Nicodemus Mkama amesema ujio wa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi,
menejimenti na timu ya wataalamu kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya
nchini Burundi umetokana na mafanikio yaliyopatikana katika masoko ya
mitaji hivi karibuni nchini Tanzania.
Ameongeza ambapo bidhaa
mpya na bunifu zinazowezesha kupata fedha za kutekeleza shughuli za
biashara na miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi
zimeidhinishwa na kuorodheshwa katika soko la hisa kwa mafanikio
makubwa.
Amesema bidhaa hizo ni pamoja na hatifungani za kijani
yaani green bond, hatifungani zenye mguso kwa jamii yaani social bonds,
na hatifungani zenye kukidhi misingi ya Shariah yaani Sukuk bonds.
“Matokeo
hayo yameiweka Tanzania katika ramani ya masoko ya mitaji ulimwenguni
yanayotoa bidhaa mpya na bunifu, zinazovutia wawekezaji wa ndani ya nchi
na kimataifa, ” amesema CPA. Mkama.
Ameeleza Masoko ya Mitaji
Tanzania ni miongoni mwa masoko yaliyopata mafanikio makubwa kiutendaji
barani Afrika, katika kipindi cha hivi karibuni. “CMSA, ambayo ni
Mamlaka yenye jukumu la kusimamia na kuendeleza masoko ya mitaji hapa
nchini …
” Imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza será na
mikakati mbalimbali ya serikali ambayo imewezesha kufikia mafanikio
hayo.Mamlaka imetekeleza mikakati ambayo imewezesha kuongeza thamani ya
uwekezaji katika masoko ya mitaji.
“Ambapo thamani ya uwekezaji
katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 7.6 na kufikia shilingi
trilioni 36.13 katika kipindi kilichoishia Novemba 2023, ikilinganishwa
na shilingi trilioni 33.59 katika kipindi kilichoishia Novemba 2022.”
Akielezea
mafanikio yaliyopatikana, CPA. Nicodemus Mkama amesema yametokana na
mazingira wezeshi, shirikishi na endelevu ya kisera, kisheria na
kiutendaji yanayotolewa na kuwezeshwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini
ya uongozi madhubuti wa Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, sera za uchumi wa kidiplomasia
na uhusiano wa kimataifa zinazotekelezwa chini ya uongozi wa Mheshimiwa
Rais Samia, zimekuwa chachu yenye matokeo chanya katika kukuza ushiriki
wa wawekezaji wa ndani na wakimataifa na hivyo kuleta mafanikio makubwa
zaidi katika masoko ya mitaji nchini Tanzania.
Hivyo kuvutia
Mamlaka za masoko ya mitaji kutoka nchni nyingine kuja kupata mafunzo
kwa lengo la kuimarisha na kuongeza ufanisi wa Taasisi katika nchi zao,
kama ambavyo CMA Burundi wamekuja kujifunza CMSA Tanzania .
CPA.
Mkama pia amesema, kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia kuhusu
tathmini ya Utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki yaani East African Common Market, Tanzania imepanda
viwango vya alama za tathmini kwa asilimia 157 kutoka alama 7 hadi alama
18 kati ya 20 na kuwa miongoni mwa nchi zinazotekelezaji vizuri itifaki
ya soko la pamoja kwenye masoko ya mitaji katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki .
Kwa sasa, Tanzania hakuna vikwazo vya ushiriki wa
wawekezaji wa kigeni katika soko la hisa, hatifungani za kampuni na
mifuko ya uwekezaji wa pamoja.
CPA. Mkama ameeleza katika kutumia
fursa ya masoko ya mitaji ya ndani na ya kimataifa yanayowezesha
kupatikana kwa fedha za kugharamia miradi na shughuli zinazochangia
Utunzaji wa Mazingira, Maendeleo ya jamii na Utawala Bora CMSA
imeidhinisha Kanuni za Soko la Hisa la Dar es Salaam yaani Stock
Exchange Rules, ili kuwezesha uorodheshwaji na mauzo ya bidhaa hizo.
Maboresho hayo yameongeza mauzo na kuweka mazingira wezeshi kwa kampuni
na taasisi kupata fedha za kugharamia shughuli za biashara na
maendeleo.Aidha maboresho hayo yameongeza matumizi ya bidhaa na huduma,
hivyo kuongeza ukwasi kwenye masoko ya mitaji.
CPA. Mkama pia
alieleza CMSA imetekeleza mkakati wa kuwezesha utoaji wa Hatifungani za
Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma ili kuwezesha Mamlaka za Serikali
za Mitaa (Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya) na Taasisi za Umma, ikiwa ni
pamoja na Mamlaka za Maji na Mazingira kugharamia miradi ya kimkakati
yenye uwezo wa kujiendesha kibiashara.
“Jitihada hizi ni sehemu
ya utekelezaji wa Mkakati wa Serikali wa njia mbadala za kugharamia
miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi uliozinduliwa na
Waziri wa.Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali
fedha kwa ajili ya kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.
“Jitihada
hizo zimeiwezesha Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la
Tanga Tanga-UWASA kuwa Taasisi ya kwanza nchini kukidhi vigezo vya awali
vitakavyoiwezesha kutoa hatifungani kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu
ya maji na utunzaji wa mazingira.
Aidha, CPA. Mkama pia alieleza
kuwa, Katika kuwezesha matumizi ya teknolojia, CMSA imeidhinisha mifumo
ya Sim Invest na Hisa Kiganjani ambayo inawezesha kutoa huduma katika
masoko ya mitaji kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano katika
kuuza na kununua dhamana.
Hatua hiyo imewezesha kuongeza ushiriki wa wananchi mijini na vijijini katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja na soko la hisa.
Aidha, CMSA imeshirikiana na wadau kuandaa miongozo ya kuendesha na
kusimamia bidhaa za mitaji halaiki yaani crowdfunding. Bidhaa hizi
zitawezesha upatikanaji wa fedha kwa kampuni changa, ndogo na za kati.
Pamoja
na hayo amesema CMSA itaendelea kujenga mazingira wezeshi na shirikishi
ili kuwezesha taasisi katika sekta ya umma na binafsi kutumia masoko ya
mitaji kupata fedha za kutekeleza miradi na shughuli za maendeleo ikiwa
ni pamoja na kuuza hisa kwa umma, hatifungani za miundombinu,
hatifungani Rafiki wa mazingira, hatifungani za bluu na hatifungani za
taasisi za Serikali.
Pia CMSA itaendelea kushirikiana na CMA –
Burundi ili kufanikisha azma ya kuwa na masoko ya mitaji imara, yenye
ufanisi na yanayochochea ukuaji wa sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla
katika jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya nchini Burundi (CMA – Burundi)
Bwa.Allisen Mgenzi ameishukuru Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana
(CMSA) Tanzania kwa kuwapokea vizuri .
Bwa. Mgenzi amesema
amekuja nchini Tanzania akiwa ameongozana na Wajumbe wa bodi ya
Wakurugenzi ya CMA-Burundi,Menejiment na timu ya Wataalamu kwa ajili ya
kufanya ziara ya Mafunzo ya siku tano katika Mamlaka ya Masoko ya Mitaji
na Dhamana (CMSA) nchini Tanzania,Soko la Hisa la Dare es Salaam
(DSE),kampuni ya Usimamizi wa Uwekezaji na Watendaji wengine katika
masoko ya mitaji.
“ziara yetu imelenga kujenga uelewa wa namna
masoko ya mitaji yanavyoendeshwa na kuainisha masuala muhimu
yatakayoiwezesha nchi ya Burundi kuwa na masoko ya mitaji
imara,himilivu,yenye ufanisi na itakayozesha kuwa na matokeo chanya
katika kuchochochea ukuaji wa sekta ya fedha na uchumi nchini Burundi
kama ilivyo nchini Tanzani”,amesema Mgenzi.
Mgenzi ameushukuru
Uongozi wa CMSA Tanzania kwa kuwapokea vizuri na kuwaonesha namna
ambavyo CMSA ilivyofanikiwa katika suala zima la kukuza soko la mitaji
nchini Tanzania,lakini pia ameishukuru Serikali ya Tanzania kuendelea
kuimarisha mahusiano mazuri na nchi ya Burundi.
Ofisa
Mtendaji Mkuu wa CMSA CPA. Nicodemus Mkama akizungumza na Waandishi wa
Habari (hawapo pichani) kuhusu kupokea ujumbe kutoka Mamlaka ya Masoko
ya Mitaji ya nchini Burundi (CMA – Burundi) unaojumuisha Wajumbe wa Bodi
ya Wakurugenzi, Menejimenti na Timu ya Wataalamu kwa ajili ya kufanya
ziara ya mafunzo ya siku tano.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya nchini Burundi (CMA –
Burundi) Bwa.Allisen Mgenzi kuhusu ujio wao kutoka Mamlaka ya Masoko ya
Mitaji ya nchini Burundi (CMA – Burundi) unaojumuisha Wajumbe wa Bodi ya
Wakurugenzi, Menejimenti na Timu ya Wataalamu kwa ajili ya kufanya
ziara ya mafunzo ya siku tano nchini Tanzania.