Featured Kitaifa

SEKTA YA WACHIMBAJI WADOGO WA DHAHABU NCHINI HUTUMIA TANI 18.5

Written by mzalendoeditor

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Bw. Edward Nyamanga akifungua Warsha ya Uhamasishaji wa Utekelezaji wa Mpango – kazi kitaifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki kwenye Uchimbaji mdogo wa Dhahabu (2020-25) iliyofanyika jijini Dodoma leo Machi 15, 2022.

Washirki wa Warsha ya Uhamasishaji wa Utekelezaji wa Mpango – kazi kitaifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki kwenye Uchimbaji mdogo wa Dhahabu (2020-25) wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Bw. Edward Nyamanga wakati akifungua warsha hiyo jijini Dodoma leo Machi 15, 2022.

Afisa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Onesphory Kamukuru akitoa neno la ukaribisho wakati wa Warsha ya Uhamasishaji wa Utekelezaji wa Mpango – kazi kitaifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki kwenye Uchimbaji mdogo wa Dhahabu (2020-25) jijini Dodoma leo Machi 15, 2022.

Washirki wa Warsha ya Uhamasishaji wa Utekelezaji wa Mpango – kazi kitaifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki kwenye Uchimbaji mdogo wa Dhahabu (2020-25) wakiwa katika picha ya pamoja na
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Bw. Edward Nyamanga wakati akifungua warsha hiyo jijini Dodoma leo Machi 15, 2022.

………………………………………

Imeelezwa kuwa sekta ya wachimbaji wadogo wa dhahabu nchini hutumia tani 18.5 za Zebaki kila mwaka bila kuzingatia tahadhari kinasi kinachoweza kuathiri afya za wananchi na mazingira hali inayoweza kuathiri ustawi wa maendeleo endelevu ya nchi yetu.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Bw. Edward Nyamanga wakati akifungua Warsha ya Uhamasishaji wa Utekelezaji wa Mpango – kazi kitaifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki kwenye Uchimbaji mdogo wa Dhahabu (2020-25) jijini Dodoma leo Machi 15, 2022.

Alisema kuwa Licha ya faida kubwa inayopatikana kutokana na sekta hii, shughuli za wachimbaji wadogo zimeibua changamoto nyingi kwa afya ya binadamu na mazingira zikiwemo umwagaji maji yenye sumu kwenye mazingira.

Pia alisema kuwa mazingira yanakabiliwa na uchafuzi wa hewa unaotokana na uchomaji holela wa dhahabu, ukataji wa miti mikubwa kupata magogo ya kujengea mashimo na wakati huo binadamu kufanya uchenjuaji wa dhahabu bila kutumia vifaa kinga unaweza kusababisha madhara ya kiafya.

“Shirika la Afya duniani (WHO), limeitaja Zebaki kuwa ni miongoni mwa vyanzo 10 hatarishi kwa afya ya binadamu na kutokana na hali hiyo, Jumuiya ya kimataifa ilipitisha Mkataba wa Minamata mwaka 2013, wenye madhumuni ya kulinda afya ya binadamu dhidi ya madhara ya uchafuzi wa mazingira unaotokana na kemikali hiyo.

“Madhara makubwa ya kiafya yatokanayo na Zebaki ni pamoja na kuathirika kwa mfumo wa neva, miguu na mikono kufa ganzi, kukosa nguvu, misuli kulegea, figo kuathirika, uono hafifu, kupoteza uwezo wa kusikia na kuongea, mimba kuharibika, kuzaa watoto wenye ulemavu wa akili, kupoteza kumbukumbu, kukosa usingizi kwa muda mrefu na kiharusi,” alitahadharisha.

Kwa upande mwingine Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kuwa katika kuhakikisha tunalinda afya ya binadamu dhidi ya madhara yatokanayo na Zebaki, Tanzania ilishiriki kikamilifu katika majadiliano ya kuanzishwa kwa Mkataba wa Minamata, kutia saini makubaliano ya Mkataba huo mwaka 2013 na kuuridhia mwaka 2020.

Kwa mujibu wa Ibara ya saba (7) ya Mkataba wa Minamata inazielekeza nchi wananchama kupunguza au kusitisha kabisa matumizi ya Zebaki, hivyo Tanzania ilitekeleza mradi wa miaka miwili wa kuandaa Mpango Kazi wa Taifa wa miaka Mitano (5) (2020-25) wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki.

Alisema mradi huu ni nyenzo mojawapo ya kupunguza na iwapo itawezekana kuondosha kabisa matumizi ya zebaki katika shughuli za uchimbaji mdogo wa dhahabu kwa kuhamasisha matumizi ya teknolojia mbadala ili kulinda afya ya binadamu na mazingira kwa ujumla. Alilishukuru Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kwa msaada wa rasilimali fedha na Utaalamu katika kufadhili mradi huo.

Warsha hiyo imeshirikisha washiriki kutoka wizara za kisekta na taasisi za Serikali zinazohusiana na shughuli za uchimbaji mdogo wa dhahabu unaotumia kemikali ya Zebaki.

About the author

mzalendoeditor