Featured Kitaifa

MAJALIWA: MASHINE ZA UKUSANYAJI WA MAPATO ZITUMIKE VIZURI

Written by mzalendoeditor

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Wakuu wa Mikoa yote Tanzani Bara kwa njia ya video, akiwa ofisini kwake, Mlimwa jijini Dodoma,  Machi 14, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

…………………………………………………..

*Awataka Watanzania wajivunie mafanikio ya mwaka mmoja ya Rais Samia

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa wahakikishe halmashauri zote nchini zinatumia vizuri mashine na mifumo iliyowekwa katika ukusanyaji wa mapato.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka wakuu wa mikoa wasimamie suala la uadilifu kwenye ukusanyaji wa mapato. “Jiridhisheni kile kinachokusanywa na kiasi kinachopelekwa ni halisi”.

“Lazima suala hili lisimamiwe kwa nguvu zote. Moja ya ajenda kubwa ni mapato, ukusanyaji wa mapato iwe ajenda namba moja katika ratiba zenu za utendaji kazi za kila siku.”

Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Machi 14, 2022) wakati akizungumza na viongozi hao katika kikao alichokiendesha kwa njia ya video kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.

Mheshimiwa Majaliwa amesema iwapo hawatasimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato bajeti zao hazitoongezeka na hivyo kuathiri utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema viongozi hao wanatakiwa wajiridhishe kama watendaji wa halmashauri wanamudu kufikia vyanzo vyote vya mapato, kuviratibu na kutumia mifumo sahihi ya ukusanyaji.

“…Msiwaachie TAMISEMI pekee kusimamia ukusanyaji wa mapato, twende tukasimamie kwenye halmashauri zetu ili kuhakikisha makusanyo hayo yanaongezeka kila siku.”

Waziri Mkuu amewataka watendaji hao wahakikishe wanasimamia vizuri miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo yao na lazima ilingane na kiwango cha fedha kilichotolewa.

Pia, amewataka Watanzania wajivunie mafanikio yaliyopatika katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassani.

About the author

mzalendoeditor