Featured Kitaifa

TANAPA KUPOKEA VIFAA VYA KISASA VYA ULINZI:WAZIRI KAIRUKI

Written by mzalendo

Na. Jacob Kasiri – Arusha.

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki amesema kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono TANAPA kuhakikisha wanapata vifaa vingi vya kisasa kwa ajili ya ulinzi wa maliasili ili kukuza utalii katika Hifadhi za Taifa.

Kikao cha Waziri Kairuki pamoja na maafisa na askari hao kimefanyika leo tarehe 28.10.2023 katika Makao Makuu ya Shirika hilo yaliyopo mtaa wa Majengo jijini Arusha.

Mhe. Kairuki alisema, “Serikali itawaunga mkono TANAPA kuhakikisha mnapata vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuimarisha doria ili uhifadhi uwe endelevu kwa manufaa ya sasa na baadae”.

“TANAPA mmepewa asilimia 10.2 ya ardhi yote ya Tanzania kuilinda na kuiendeleza. Katika eneo hilo tuhakikishe hakuna uvamizi wa makazi wala mifugo”, aliongeza Mhe. Kairuki.

Waziri Kairuki pia, amelitaka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuendelea kuimarisha ujirani mwema kwa vijiji vinavyozunguka hifadhi ili kuwa na uhifadhi wa pamoja na kupunguza migogoro baina ya wananchi na hifadhi.

Aidha, Mhe. Kairuki ametoa wito kwa Watanzania na wasio watanzania kujitokeza kushiriki katika tukio la kupanda Mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Taifa la Tanzania.

Waziri huyo alisema, “ninawaomba watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la kupanda Mlima Kilimanjaro, zoezi hilo huwa linaongozwa na JWTZ na wenzetu wa TANAPA. Najua mwaka jana kulikuwa na wapandaji zaidi ya 200, mwaka huu tutavunja rekodi kutokana na kampuni zilizopewa dhamana ya kupandisha watu mlimani kuwa 3 tofauti na mwaka jana ilikuwa ni kampuni 1 tu”.

Kaimu Kamishna wa Uhifadhi TANAPA -Juma Kuji alisema kuwa ziara ya Waziri wa Maliasili na Utalii imekuwa na tija kwa kuendelea kutusisitiza tufanye kazi kwa bidii na kwa kufuata sheria na taratibu.

Kamishna Juma alisema, “kwa niaba ya maafisa na askari wa TANAPA tunakupongeza kwa kuteuliwa kwako na Mhe. Rais na tunakuahidi kuwa maelekezo yako tutayatekeleza ili kuendeleza uhifadhi na kukuza utalii nchini”.

Katika ziara hiyo Waziri Kairuki ameweka wazi nia na mpango wake wa kutembelea Hifadhi zote za Taifa ili kujionea vivutio vya utalii na kuzungumza na watumishi.

About the author

mzalendo