Mhifadhi Mkuu anayesimamia Kitengo cha Dawati la Ujirani Mwema kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) PC Twaha Twaibu
Na.Alex Sonna-DODOMA
MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imewataka wananchi kuacha tabia ya kujenga makazi au kufanya shughuli za kibinadamu karibu na hifadhi za wanyamapori ili kujiepusha na hatari za wanyama wakali.
Kauli hiyo imetolewa na Mhifadhi Mkuu anayesimamia Kitengo cha Dawati la Ujirani Mwema kutoka TAWA PC Twaha Twaibu wakati akiongea kwa njia ya simu na Mtandao wa Mzalendo blog ,ambapo amesema kuwa jamii inatakiwa kuelewa kuwa kujenga karibu na hifadhi za wanayampori ni kuhatarisha maisha yao.
PC Twaha ameitaka jamii kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalam wa Wanyamapori ili kuepuka athari zitokanazo na wanyama wakali na waharibifu kama Tembo,Nyati,Mamba,Kiboko na wengineo.
Amesema baadhi ya maeneo hapa nchini yalikuwa ni mapitio ya Wanyamapori kipindi cha nyuma na wanyama hao huwa na tabia ya kurejea katika maeneo hayo haswa Tembo hivyo jamii inatakiwa kuwa makini kwa kutowakaribia.
“Kuna wakati wanyama wanafika hadi kwenye makazi ya watu, ukiona mnyamapori kwenye mazingira unayoishi toa taarifa kwa haraka kwa viongozi wa maeneo unayoishi ili hatua za kiusalama ziweze kuchukuliwa na wataalam wa Wanyamapori ambao ni TANAPA na TAWA.
“Tumesomea namna ya kuwadhibiti pia kuna tabia ya baadhi ya wananchi kutaka kupiga picha nao kitendo hicho kinahatarisha maisha yao”, amesema PC Twaha.
Amewashauri wananchi wenye umri mkubwa na waliotumia vilevi kutokufukuza wanyama hao na kutofanya shughuli za kibinadamu katika mapitio ya Wanyamapori.
Hata hivyo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara katika Utalii,Uhifadhi na ndie aliezindua Jeshi la Uhifadhi (USU)wakati alipokuwa Makamu wa Rais.
TAWA kupitia kitengo chake cha uelimishaji imefanikiwa kutoa elimu kwa wananchi wapatao laki Saba na sita elfu na mia tatu kupitia mikutano 1925 katika maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake Afisa Wanyamapori kutoka TAWA Joseph Mnyai ameelezea faida zinazotokana na Uhifadhi kupitia uwindaji wa kutalii na utalii wa picha kuwa ni upatikanaji wa fedha za kigeni.
Fedha hizo hupelekwa kuchangia shughuli za maendeleo katika jamii zilizopo kandokando mwa mbuga hizo yakiwemo mapori ya akiba tengefu na maeneo ya ardhi oevu kwa kuzingatia utaratibu wa mamlaka.