Featured Kitaifa

MHE FATMA TOUFIQ AWATAKA WANAWAKE NCHINI WENYE UMRI WA KUZAA KUWAHI HOSPITALI NA KUPIMA AFYA ZAO

Written by mzalendoeditor
NA. Majid Abdulkarim, Mwanza
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maswala ya UKIMWI,Kifua Kikuu, Madawa ya Kulevya n inayoongozwa na Mhe. Fatma Toufiq imewataka wanawake nchini wenye umri wa kuzaa kuwahi hospitali na kupima afya zao pale wanapopata ujauzito ili watakapo kutwa na maambukizi yoyote kuanza dawa mara moja ili kumkinga mtoto atakayezaliwa.
Mhe. Toufiq ameweka bayana kuwa akinamama wakiwahi hospitali itasaidia kuzuia maambukizi kwa Watoto kipindi watakapo kuwa wamezaliwa kwani mama akipima afya yake akakutwa na maambukizi ataweza patiwa tiba kwa wakati.
Mhe. Toufiq ametoa wito huo leo wakati kamati hiyo ilipofanya ziara yake katika mwalo wa Kirumba Mkoani Mwanza ambapo amesema kuwa kila mtu akichukua hatua  kwa kutimiza wajibu wake, ushirikiano thabiti, elimu ikiendelea kutolea wataweza kufikia malengo ya kutokomeza UKIMWI,Kifua Kikuu nchini na dawa za kulevya.
Mhe. Toufiuq amesema kuwa Tanzania bila Maambukizi mapya ya UKIMWI inawezekana, Tanzania bila maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto inawezekana na Tanzania bila Kifua kikuu inawezekana.
“Wazazi katika kaya zetu tuwaelekeze vijana wetu kuacha kutumia dawa za kulevya na kwa kufanya hivyo ipo siku dawa za kulevya zitakuwa historia nchini, naamini Tanzania bila dawa za kulevya inawezekana”, ameeleza Mhe. Toufiq
Mhe. Toufiq amesema kuwa wao kama wabunge wanaendelea kutoa shime na kushauri wananchi wote kuendelea kufanya upimaji wa afya zao na zoezi hili la upimaji wa afya za wananchi katika maeneo ya kutolea huduma za jamii ni endelevu ili wananchi kuwa na afya bora katika utafutaji wao wa kila siku.
Aidha, Mhe. Toufiq amewaasa wanaume kufanya tohara ili kuhakikisha wanakuwa na afya bora na kupunguza maambukizi ya UKIMWI nchini.
“Lakini pia wazazi tujenge utamaduni wa kufanyia Watoto wetu tohara wakati wakiwa wadogo ili kupunguza maambukizi katika jamii zetu pale wanapokuwa wakubwa”, amesisitiza Mhe. Toufiq
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Ngusa Samike ameishukuru kamati hiyo kwa ziara yake katika mkoa huo ambapo amesema kuwa ziara ya kamati hiyo imekuwa na tija kwa watendaji wa mkoa huo kwani imepata kuibua mambo mbali mbali katika mkoa huo mbayo yanatakiwa kufanyiwa kazi ili kuzuia  maambukizi mapya ya ukimwi, kifua kikuu na mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Naye mmoja wa wafanya Biashara katika mwalo wa Kirumba Geofery Ndagabona ametoa wito kwa uongozi wa mkoa kuwa zoezi la upimaji wa afya liwe endelevu ili kusaidia wananchi wa mkoa huo kujua afya zao mara kwa mara na kupunguza maambukizi mapya.

About the author

mzalendoeditor