Featured Kitaifa

VIJANA WA TANZANIA WALIOKUWA KWENYE MAFUNZO YA KILIMO CHA KISASA NCHINI ISRAEL WANG’ARA

Written by mzalendoeditor

Vijana
99 kati ya vijana 100 waliokuwa wanapatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa
njia ya vitendo katika Kituo cha Kimataifa cha mafunzo ya Kilimo cha Arava kilichopo
Kusini mwa Israel, wamehitimu mafunzo na kutunukiwa vyeti katika mahafali yaliyofanyika
tarehe 12 Juni 2023 (The Arava International Center for Agriculture Training –
AICAT).

 

Kundi
hili la watu 99 ambaye mmoja alirejeshwa nchini kutokana na changamoto za
kiafya ni la kwanza kuhitimu katika kituo hicho tangu Tanzania ilipojiunga kwa
mara ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2022/2023.

 

Katika
hotuba yake, Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Alex Kallua aliwapongeza
wahitimu wote na kuwaasa kuwa chachu ya mabadiliko wanaporejea nchini kwao kwa
kufanyia kazi kwa vitendo mafunzo waliyoyapata nchini Israel.

 

Katika
mahafali hayo, mradi mmoja kutoka kwa vijana wa Tanzania ulishinda tuzo ya Dola
za
Marekani 6,000.00 kutoka kwa The Dean Family Fellowship Grant, kufuatia
shindano la kuandika na kuwasilisha mradi ambao vijana husika watafanya na
kuleta mabadiliko chanya kwao na kwa jamii inayowazunguka, mara baada ya
kurejea nyumbani. Tuzo hii itawawezesha vijana walioshinda kuanzisha mradi
husika na hivyo kujikwamua kiuchumi. Shindano lilihusisha nchi 12 ambazo
zinashiriki mafunzo hayo na tuzo ilitolewa kwa nchi 7 ikiwemo Tanzania.

 

Aidha,
vijana 5 kutoka Tanzania walipata tuzo ya wanafunzi bora na kijana mmoja ambaye
alikuwa kiongozi wa kundi la Tanzania amepewa ofa ya kuendelea na mafunzo kwa
mwaka ujao wa masomo kutokana na nidhamu na uongozi uliotukuka.

 

Kwa
mwaka wa masomo 2022/2023, Tanzania ilipewa nafasi za masomo 250 ambapo vijana
100 walipelekwa kwenye kituo cha AICAT na 150 walipelekwa kituo cha mafunzo cha
Agrostudies ambacho kimekuwa kikitoa mafunzo hayo kwa vijana wa Tanzania tangu
programu hii ilivyoanza. Vijana wengine 150 wanatarajiwa kuhitimu mafunzo yao
mwezi Agosti 2023.

 

Kwa
mwaka wa masomo 2023/2024, Tanzania imepewa nafasi 260 ambapo vijana 150
watapelekwa Agrostudies na vijana 110 watapelekwa AICAT.

Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Alex Kallua akimtunuku cheti mmoja wa mhitimu wa mafunzo ya kilimo kwa vitendo nchini Israel 
Mhitimu wa wa mafunzo ya kilimo kwa vitendo nchini Israel baada ya kutunukiwa cheti na Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Alex Kallua

Wahitimu wa mafunzo ya kilimo kwa vitendo wakiwa na vyetu vyao baada ya kutunukiwa wakati wa mahafali yaliyofanyika nchini Israel tarehe 12 Juni 2023.
Usawa wa kijinsia umezingatiwa, Mhitimu wa Kike wa Mafunzo ya kilimo kwa vitendo nchini Israel akitunukiwa cheti na Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Alex Kallua

Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe. Alex Kallua akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wakiwa wameshikilia mfano wa hundi ya Dola za Marekani 6000 kufuatia ushindi walioupata kwenye shindano la Andiko Mradi

About the author

mzalendoeditor