Featured • Kitaifa

RC SENYAMULE:MJI WA SERIKALI MTUMBA KUCHOCHEA UCHUMI WA DODOMA

Written by Alex Sonna

 

Na.Erick Nenda-DODOMA

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema kukamilika na kuanza kutumika kwa Mji wa Serikali Mtumba kutachochea ukuaji wa uchumi wa mkoa huo kupitia ongezeko la fursa za biashara, ajira, uwekezaji na utalii, huku kukitarajiwa kufungua maeneo mapya ya maendeleo ndani ya Jiji la Dodoma.

Mhe.Senyamule ameyasema hayo leo Oktoba 27,2026 wakati akikagua maandalizi ya uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba unaotarajiwa kuzinduliwa Oktoba 30,2026 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Amesema ujenzi wa mji huo wenye majengo ya kisasa ya wizara na taasisi za Serikali ni hatua muhimu katika kuimarisha hadhi ya Dodoma kama makao makuu ya nchi, akitoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukamilisha mradi huo na kuwezesha watumishi kuhamia na kuanza kutoa huduma katika eneo hilo.

“Ujenzi wa Mji wa Serikali tayari umechangia shughuli za kiuchumi kwa wananchi kupitia ajira na biashara mbalimbali, hata kabla ya kukamilika kwake, huku matumizi ya majengo hayo yakitarajiwa kuongeza mahitaji ya bidhaa na huduma zitakazotolewa na wajasiriamali wa ndani.”amesema Senyamule

Ameeleza kuwa uwepo wa wizara na taasisi za Serikali katika eneo moja utatoa fursa kwa wafanyabiashara wanaotoa huduma za chakula, usafi, usafirishaji na bidhaa nyingine zinazohitajika na watumishi pamoja na wageni watakaotembelea mji huo. Amesema fursa hizo zinapaswa kutumiwa na wananchi kwa kuanzisha na kuimarisha biashara zenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya eneo hilo.

Aidha, amesema Mji wa Serikali Mtumba unatarajiwa kuchochea upanuzi wa Jiji la Dodoma kwa kufungua eneo jipya la makazi na shughuli za kiuchumi, hatua itakayosaidia kupunguza msongamano wa shughuli katikati ya jiji na kuongeza mahitaji ya huduma muhimu kama afya, elimu, biashara na makazi.

Ameongeza kuwa ongezeko la watu watakaofanya kazi na kuishi Mtumba litatoa nafasi kwa wawekezaji kuanzisha miradi mipya itakayosaidia kukuza uchumi wa eneo hilo.

Senyamule amesema uwekezaji huo pia umeambatana na ujenzi na uboreshaji wa miundombinu muhimu, ikiwemo barabara, umeme na huduma za maji, ambayo inaweza kunufaisha wananchi wanaoishi Mtumba na maeneo jirani.

Ameeleza kuwa miundombinu hiyo ikiendelea kuimarishwa, itasaidia kuvutia uwekezaji zaidi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakazi wa maeneo yanayozunguka mji huo.

Katika hatua nyingine, amesema Mkoa wa Dodoma umejipanga kuutangaza Mji wa Serikali kama sehemu ya vivutio vya utalii wa ndani kupitia ziara za kutembelea jiji (city tours), ili wananchi na wageni waweze kujionea uwekezaji uliofanyika.

Amesema mpango huo utasaidia kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea Dodoma na kutoa fursa kwa sekta nyingine, ikiwemo hoteli, usafiri, migahawa na biashara za huduma, kunufaika kiuchumi.

Hata hivyo, Senyamule amesisitiza umuhimu wa kutunza mazingira na kudumisha usafi ili kuendana na hadhi ya majengo na miundombinu ya kisasa iliyojengwa Mtumba.

Amesema mkoa una mpango wa kuongeza maeneo ya kijani na kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika usafiri, ikiwemo magari, pikipiki na bajaji, huku akiwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya uzinduzi wa Mji wa Serikali na kutumia fursa zinazotokana na uwekezaji huo kwa maendeleo yao na ya mkoa kwa ujumla.

About the author

Alex Sonna