WAZIRI wa Katiba na Sheria, George Simbachawene,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo March 3,2022 jijini Dodoma kuhusu Kikao cha 49 cha Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu alikichofunguliwa Februari 28, mwaka huu na yeye alihutubia Baraza hilo Machi 2, mwaka huu kwa njia ya video.
…………………………………………..
Na Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Katiba na Sheria, George Simbachawene,amesema kuwa Tanzania inatambua wajibu wake mkuu wa kulinda na kukuza haki za binadamu kama mwanachama wa Umoja wa Taifa (UN) na Baraza la Haki za Binadamu.
Hayo ameyasema leo March 3,2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Kikao cha 49 cha Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu alikichofunguliwa Februari 28, mwaka huu na yeye alihutubia Baraza hilo Machi 2, mwaka huu kwa njia ya video.
Simbachawene amesema kuwa Serikali ipo imara na inafanya jitihada za makusudi kuhakikisha haki za msingi na uhuru wa kidemokrasia, haki za kiraia na za kisiasa zinaheshimiwa na pia kuna mazingira wezeshi ya kukuza haki za kisiasa nchini.
“Rais Samia Suluhu Hassan alifungua kikao cha majadiliano Desemba mwaka jana baina ya viongozi wa juu serikalini na wa vyama vya siasa na wadau wa utawala bora na demokrasia nchini ikiwa ni kuhakikisha haki za msingi na uhuru wa demokarasia zinaendelezwa nchini,”amesema Simbachawene
Katika kuendeleza haki ya kupata taarifa na uhuru wa kutoa maoni nchini, Serikali imekuwa na majadiliano wazi na vyombo vya habari na wanahabari. Majadiliano hayo yamekuwa na mafanikio makubwa na hata kusababisha runinga za mtandaoni kufunguliwa pamoja na baadhi ya magazeti yaliyokuwa yamefungiwa kufunguliwa na kuendelea na kazi. Na bado majadiliano kuhusu namna ya kupitia sheria ya habari na haki za wanahabari yanaendelea.
Serikali haifanyi kazi ya kukuza na kulinda haki za binadamu kwa kujifungia peke yake, inafanya kwa ushirikiano na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Asasi Zisizo za Serikali na wadau wa Maendeleo ambao wana maono sawa na ya serikali kuhusu kukuza na kulinda haki za binadamu kwa wananchi.
‘Serikali ina kazi kubwa kuhakikisha kwamba haki za mtu mmoja au jamiii haisababishi mtu mwingine au jamii kunyimwa haki. Hivyo, itaendelea kuhakikisha kwamba sheria, Sera, mipango, mikakati na uamuzi wake unazingatia misingi ya haki za binadamu ambayo ni usawa na kutobaguliwa’amesema
Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kusimamia wajibu wa Serikali wa kukuza na kulinda haki za binadamu kama ilivyobainishwa kwenye katiba, sheria na mikataba ya kimataifa na kikanda ya haki za binadamu ambayo Serikali imeridhia.
Hata hivyo ameeleza hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali katika kupambana na Uviko-19 na kuifanya nchi kupata mkopo nafuu wa Sh.trilioni 1.3 wa kupunguza makali ya athari ya ugonjwa huo katika sekta mbalimbali zikiwemo za afya, elimu, maji na katika makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Aidha Simbachawene amesema kuwa kati ya sheria 450 zilizokuwa zikitumika mahakamani kwa Kiingereza tayari 300 zimetafsiriwa kwa Kiswahili sawa na asilimia 80.
“Suala la kutafsiri sheria hizi linaenda vizuri hata kama kuanza kuzitumia linahitaji kukaa pamoja na mahakama ili kukubaliana lini zianze kutumika rasmi katika mhimili wa mahakama kwa lengo la kusaidia wananchi kupata haki kutokana na kutumika Kiswahili katika kutoa uamuzi au hukumu,”amesema