Featured Kitaifa

WAZAZI WAPENI WATOTO ELIMU YA MAKUZI,AFYA YA UZAZI-MRAJIS

Written by mzalendoeditor

 

MRAJISI wa Asasi za Kiraia Zanzibar, Ahmed Abdulla (wa pili kushoto) akimkabidhi mmoja ya wanafunzi wa skuli ya St. Paul Kiungani wakati wa zoezi la ugawaji wa taulo za kike kwa wanafunzi zilizotolewa na taasisi ya Women and Children Support Association (WCWSA) kwa kushirikiana na wadau wengine skulini hapo jana.

MMOJA ya wanafunzi wa skuli ya sekondari St. Monica akitoa maelezo ya ufahamu wake juu ya masuala ya hedhi salama wakati wa zoezi la ugawaji wa taulo za kike kwa wanafunzi zilizotolewa na taasisi ya Women and Children Support Association (WCWSA) kwa kushirikiana na wadau wengine lilifanyika katika skuli ya St. Paul Kiungani mjini Unguja.

Baadhi ya wadau wa shirika la Women and Children Welfare Support Association (WCWSA), wakiwa na mgeni rasmi Mrajisi wa Asasi za Kiraia Zanzibar, Ahmed Abdulla, baada ya uzunduzi wa zoezi la ugawaji taulo za kike kwa wanafunzi wa skuli za St. Paul na St. Monica, lililofanyika Kiungani Kilimani mjini Unguja

…………………………..

NA MWANDISHI WETU

WAZAZI wametakiwa kutofumbia macho elimu ya kujitambua, makuzi na afya ya uzazi kwa watoto wao ili kuwalinda na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika jamii.

Wito huo umetolewa na Mrajisi wa Asasi za Kiraia Zanzibar, Ahmed Abdallah, alipokua akizindua zoezi la ugawaji wa taulo za kike na elimu ya hedhi salama kwa wanafunzi wa skuli za St. Paul na St. Monica, lililofanyika Kiungani mjini unguja.

Alieleza kuwa ukimya uliopo kwa baadhi ya wazazi juu ya masuala ya mabadiliko ya kimaumbile ya watoto wao, hupelekea madhara yakiwemo ya kiafya jambo linaloweza kudhibitiwa kwa kujenga ukaribu na kuwapa elimu kulingana na umri na nafasi ya mtoto.

Aidha alipongeza juhudi zinazochukuliwa na asasi za kiraia ikiwemo ya Women and Children Welfare Support Association (WCWSA), Holding Hands Foundation na WAJAMAMA kwa kutoa elimu inayohusu hedhi salama na kugawa taulo hizo kwa wanafunzi jambo litakaloongeza ufanisi wao masomoni.

“Tukiacha watoto wetu wajifunze au wafundishane wenyewe kwa wenyewe tunaweza kuwa na jamii yenye uelewa potofu juu ya hii dhana, hivyo nazishukuru taasisi zilizojipa wajibu wa kuisaidia serikali kutimiza lengo la kuimarisha ustawi wa jamii na maendeleo ya nchi yetu,” alieleza Ahmed.

Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inathamini mchango unaotolewa na Asasi za Kiraia ambao alisema unaziba pengo la kiutekelezaji wa majukumu ya serikali na kuzitaka kufanya kazi kulingana na malengo ya kuanzishwa kwao na mahitaji ya jamii.

“Natoa wito kwa Asasi za Kiraia kuendelea kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia sheria za nchi, lakini pia mila na desturi za watu wa Zanzibar na ofisi yangu ipo tayari wakati wote kuzisaidia,” alifafanua Mrajis.

Awali Katibu wa Kanisa la Anglican Zanzibar, Padri Stanley Lichinga, alipongeza usimamizi na ufuatiliaji unaofanywa na ofisi ya mrajisi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali kwani yamekua msaada mkubwa kwa jamii.

Aidha aliitaka jamii hasa wanaume kuwa karibu na watoto wao wa kike kuwasikiliza na kuwapa njia za kujilinda dhidi ya changamoto mbali mbali zilizomo katika jamii.

“Zamani tulikua na mambo ya kimila ambayo yaliwawezesha wasichana wanapokua wakubwa kupata uelewa juu ya masuala ya makuzi yao lakini sasa hayapo sasa pamoja na hizi asasi kubeba wajibu huo, wazazi hasa wanaume tunapaswa kuwa sehemu ya darasa kwa watoto wetu wote,” alieleza Padri Lichinga.

Akizungumzia zoezi hilo, Afisa Miradi wa WCWSA, Ester Mwakarobo, alieleza kuwa zoezi hilo ni endelevu na kwamba litafanyika katika skuli nyengine za Unguja na pemba.

Aliongeza kuwa katika mpango kazi wa shirika hilo, mbali ya kutoa elimu ya kuhusu hedhi salama na kugawa taulo za kike, pia lina mpango wa kusaidia upatikanaji wa huduma muhimu katika skuli zikiwemo za maji safi na salama na chakula kwa wanafunzi.

“WCWSA imejikita zaidi kukabiliana na changamoto zinazowagusa watoto na wanawake na ndio maana katika mpango kazi wetu tunatarajia kuzifikia skuli na kutoa chakula angalau mlo mmoja ili kuhamasisha watoto kupenda kusoma na kuongeza ufaulu,” alieleza Mwakalobo.

Nae Mwenyekiti wa Holding Hands Foundation, Florence Robert, aliahidi kuwa wataendelea kutoa elimu juu ya usafi na hedhi salama kwa wasichana na wanawake ili kuwa na jamii salama dhidi ya maradhi yanayotokana naafya ya uzazi.

Aliongeza kuwa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, shirika lake limeifikia jamii hasa wenye mahitaji maalum kwa kuwaunganisha na wafadhili waliowapatia misaada inayowaondolea changamoto wanazopitia.

Nae mmoja ya wadau waliosaidia upatikanaji wa vifaa hivyo, Sasha Sarafin kutoka Sasha Tours alitoa rai kwa serikali kutenga bajeti ya taulo za kike na elimu ya afya kwa wasichana walioko skuli ili kuwaongezea hali ya kujiamini na kufanya vyema kwenye masomo yao.

“Kwa muda mrefu taasisi za kiraia zimekua zikishirikiana na serikali kutoa elimu juu ya masuala haya baada ya kuona wanawake na wasichana wengi hawana elimu ya kutosha juu ya matumizi ya vifaa vya kujihifadhia wanapokua kwenye siku zao lakini hiyo haitosh, mamlaka lazima zitenge fedha,” alieleza Sasha.

Katika tukio hilo mashirika mbali mbali yalitoa elimu ya kujitambua, usafi na hedhi salama iliyoambatana na ugawaji wa taulo za kike pamoja na namna bora ya kuzitumia bila ya kuwaathiri na kuathiri mazingira.

About the author

mzalendoeditor