Featured Kitaifa

WAZIRI MABULA ASITISHA VIBALI VYA UJENZI WA VITUO VYA MAFUTA NCHINI

Written by mzalendoeditor

 

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk.Angeline Mabula,akizungumza  na waandishi wa habari kuhusu kusitisha utoaji wa vibali vipya vya ujenzi wa vituo vya mafuta na mabadiliko ya matumizi ya ardhi kwa ajili ya vituo vya mafuta kwa muda wa miezi mitatu kuanzia leo Novemba 10,2022 jijini Dodoma.

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk.Angeline Mabula,akimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Allan Kijazi akizungumza mara baada ya kutoa taarifa kuhusu kusitisha utoaji wa vibali vipya vya ujenzi wa vituo vya mafuta na mabadiliko ya matumizi ya ardhi kwa ajili ya vituo vya mafuta kwa muda wa miezi mitatu kuanzia leo Novemba 10,2022 jijini Dodoma.

…………………………………..

Na Alex Sonna-DODOMA

SERIKALI imesitisha utoaji wa vibali vipya vya ujenzi wa vituo vya mafuta na mabadiliko ya matumizi ya ardhi kwa ajili ya vituo vya mafuta kwa muda wa miezi mitatu kuanzia leo Novemba 10,mwaka huu ili Wizara zinazohusika zifanye tathmini ya kina.

Hayo yamesemwa leo Novemba 10,2022 jijini Dodoma na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk.Angeline Mabula,wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa   kuna ujenzi holela wa vituo hivyo visivyozingatia matakwa ya sheria ya Mipangomiji na kanuni zake ikiwamo Jiji la Dar es salaam, Mkoa wa Pwani

Waziri Mabula amesema  kumekuwepo na hujenzi holela wa vituo vya mafuta nchini usiozingatia  matakwa ya Sheria ya Mipangomiji  na Kanuni zake jambo linalochagiza uwepo wa agizo hilo la kusitisha vibali hivyo.

“Ongezeko hili limeleta malalamiko mengi kutoka kwa wadau mbalimbali na kutishia ustawi sawia wa uendelezaji wa Miji na matumizi ya huduma za vituo vya mafuta,”amesema Dk.Mabula

Aidha Waziri Mabula amesema kuwa baadhi ya wamiliki wamekuwa wakiomba vibali vya ukarabati wa majengo chakavu mijini na baadae kufanya uendelezaji wa Maeneo hayo kinyume mipango kabambe iliyopo.

”Naelekeza kusitisha kutoa vibali vya ujenzi vinavyokiuka Mipango kabambe wa Majiji, Manispaa, Miji na kusitisha ugawaji viwanja kiholela unaopelekea taswira ya miji yetu kuharibika akisisitiza kuwa kama kuna mpango wa kujenga magorofa eneo husika ufuatwe mpango uliopo.”amesema

Aidha Dkt. Mabula amezitaka mamlaka za upangaji kuhakikisha uendelezaji upya maeneo ya ndani ya miji na mgawanyo wa maeneo unaofuata Mipango Kabambe iliyopo na mipango kina iliyoandaliwa.

Hata hivyo ametoa maagizo kwa wataalamu katika ofisi za ardhi kote nchini zisimamiwe utekelezaji wa Mipango Kabambe  na kuwe na ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha mapendekezo ya mipango hiyo yanatekelezwa.

Aidha Waziri Mabula ametoa wito kwa wananchi kufuata sheria,kanuni na taratibu za ujenzi zilipo nchini ili kujiepusha na ujenzi holela.

About the author

mzalendoeditor