Featured Kimataifa

DKT.MPANGO:’MATAIFA YA AFRIKA KUNUFAIKA ZAIDI NA UKANDA HURU WA KIBIASHARA’

Written by mzalendoeditor

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango akizungumza  na wawekezaji , viongozi wa sekta binafsi na umma , viongozi mbalimbali wa nchi za Afrika pamoja na washiriki wa Jukwaa la Uwekezaji Barani Afrika wakati wa Ufunguzi wa Jukwaa hilo leo tarehe 02 Novemba 2022 Jijini Abidjan nchini Ivory Coast.

……………………………..

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango amesema mataifa ya Afrika yanaweza kunufaika zaidi na ukanda huru wa kibiashara wa Afrika kwa kujenga miundombinu ya pamoja ya kikanda ili kurahisisha biashara na usafirishaji kama ilivyo dhamira ya Tanzania ya ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Tanzania hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia nchini Burundi. 

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 02 Novemba 2022 wakati wa Ufunguzi wa Jukwaa la Uwekezaji Afrika kwa mwaka 2022 linalofanyika Jijini Abidjan nchini Ivory Coast. Amesema ni muhimu pia kuondolewa vikwazo vya usafirishaji wa bidhaa na watu baina ya taifa moja na jingine pamoja na kujenga mifumo imara ya kifedha ya pamoja.

Aidha Makamu wa Rais amesema nchi za Afrika zinapaswa kujiandaa kwa kujijengea uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kuwaamini na kuwatumia wanasayansi waliopo barani Afrika pamoja na kutafuta masuluhisho ya pamoja ya ndani ya bara hilo katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko yanayoweza kujitokeza.

Halikadhalika amesema kutokana na migogoro ya kimataifa, nchi za Afrika zinaweza kutumia fursa hiyo kuwa bara tegemeo la chakula kutokana na uwepo wa mazingira rafiki na ardhi nzuri ya kilimo. Ametaja juhudi za Tanzania katika kuinua kilimo ikiwemo  uzalishaji wa mbegu za mazao ya kimkakati ili kuepukana na kuagiza kutoka mbegu hizo mataifa ya nje.

Kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, Makamu wa Rais amesema licha ya kuweka msisitizo katika upandaji wa miti , Afrika haina budi kushirikiana katika matumizi ya utajiri wa nishati mbadala iliopo ikiwemo gesi asilia ili kuepukana na uharibifu wa mazingira na ukataji miti ovyo. 

Pia amewakaribisha wawekezaji nchini Tanzania na kuwahakikishia mazingira rafiki pamoja na utajiri wa rasilimali iliojaaliwa Tanzania. Makamu wa Rais amesema ipo haja ya kushirikiana katika matumizi ya rasilimali ziliozopo barani Afrika kama vile gesi iliopo nchini Tanzania inayoweza kukidhi mahitaji ya mataifa Jirani  na hivyo kuongezeka kwa nishati mbadala itakayolinda mazingira.

Awali akitoa hotuba wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Uwekezaji Barani Afrika kwa mwaka 2022 Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambao ni waratibu wa Jukwaa hilo Dkt. Akinwumi Adesina amesema Afrika ni bara pekee lenye uhakika katika uwekezaji kutokana na uwepo wa malighafi za kutosha, Gesi asilia na Nishati ya umeme jua. Amesema takwimu zinaonesha kwamba  ifikapo mwaka 2050  , Afrika inakadiriwa kuwa na idadi ya robo ya watu duniani hivyo kuwezesha upatikanaji wa masoko ya uhakika na rasilimali watu.

Aidha Dkt.Adesina ametaja faida zingine zinazopatikana Afrika ikiwemo utajiri wa madini ya lithium na cobalt yanayotumika katika utengenezaji wa magari ya umeme yanayopatikana katika bara hilo. Amesema Ukanda huru wa biashara barani Afrika ni ukanda mkubwa zaidi duniani unaounganisha uchumi wa zaidi ya dola za marekani trioni 3.3 hivyo Afrika haiwezi kuachwa katika uwekezaji.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango akizungumza  na wawekezaji , viongozi wa sekta binafsi na umma , viongozi mbalimbali wa nchi za Afrika pamoja na washiriki wa Jukwaa la Uwekezaji Barani Afrika wakati wa Ufunguzi wa Jukwaa hilo leo tarehe 02 Novemba 2022 Jijini Abidjan nchini Ivory Coast.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango akisikiliza viongozi mbalimbali wakati wakitoa hotuba za ufunguzi katika Jukwaa la Uwekezaji Barani Afrika leo tarehe 02 Novemba 2022 linalofanyika Jijini Abidjan nchini Ivory Coast.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wakuu wa nchi na serikali kutoka baadhi ya mataifa ya Afrika pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Dr. Akinwumi A. Adesina (watatu kutoka kushoto) mara baada ya kumalizika kwa ufunguzi wa Jukwaa la Uwekezaji Barani Afrika leo tarehe 02 Novemba 2022 linalofanyika Jijini Abidjan nchini Ivory Coast.

About the author

mzalendoeditor