Featured Kitaifa

TMA YAENDELEA NA UTEKELEZAJI MRADI WA RADA,VIFAA NA MIUNDOMBINU YA HALI YA HEWA

Written by mzalendoeditor

MKURUGENZI Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Hamza Kabelwa ,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Novemba 2,2022 jijini Dodoma.

………………………….

Na Alex Sonna-DODOMA

MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imeendelea na utekelezaji wa mradi wa Rada, vifaa na miundombinu ya hali ya hewa ikiwemo kukamilika kwa asilimia 90 ya utengenezaji wa mtambo wa rada mbili za Mbeya na Kigoma.

Hayo yamesemwa na ,Mkurugenzi Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Hamza Kabelwa ,wakati akizungumza na waandishi wa habari  kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Novemba 2,2022 jijini Dodoma.

Dk Kabelwa amesema kuwa  kukamilika kwa asilimia 90 ya utengenezaji wa mtambo wa rada mbili  za Mbeya na Kigoma ambapo pia malipo ya asilimia 90 yalifanyika

“Kwa sasa TMA tuna rada tatu zilizopo katika Jiji la Dar es Salaam, Mwanza na Mtwara ambazo zinafanya kazi ya kukusanya data za hali ya hewa zinazoonesha uhalisi wa anga la Tanzania, na kwa sasa tumefikia asilimia 90 za ujenzi wa rada zingine mbili Mkoani Mbeya na Kigoma,”Amesema Dk Kabelwa

Pia mafunzo kwa wahandisi na waendesha mitambo kuhusu kuzihudumia na kuzitumia rada hizo yalifanyika kiwandani nchini Marekani.

Dk Kabelwa amesema, mamlaka hiyo katika mwaka huo 2021/22 iliendelea na utengenezaji wa rada mbili zitakazofungwa katika Kiwanja cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) na Jijini Dodoma umefikia asilimia 45.

Pia mamlaka hiyo ilifungua barua za dhamana kwa ajili ya malipo ya asilimia 80 ya kutengeneza rada hizo. Kukamilika kwa rada hizi kutakamilisha mtandao wa rada nchini wa kuwa na idadi ya rada saba.

”Kukamilika kwa Rada hizi kutakamilisha mtandao wa Rada nchini kwa idadi ya Rada saba. Rada hizi zinauwezo wa kuona zaidi ya kilometa za mkato 450 huku zikizunguka na kuona matone madogo sana ya mvua katika hali ya uhalisia ndani ya kilometa 250.”amesema Dk Kabelwa 

Aidha, mitambo hii pia inasaidia katika kukusanya data za hali ya hewa zinazoonesha uhalisi wa anga letu la Tanzania.

Hata hivyo amesema kuwa Kufungwa kwa mitambo miwili ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe inayohamishika na “measuring cylinders zipatazo 100, seti tano za vifaa vya kutambua matukio ya radi, vifaa 15 vya kupima mgandamizo wa hali ya hewa, vifaa 25 vya kupima kiasi cha joto na unyevunyevu, mitambo minne ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe na vifaa vya kupima mvua vinavyojiendesha vyenyewe.

”Mamlaka imepokea kompyuta maalum Cluster Computer ambayo ipo katika hatua ya ufungaji. Vilevile Mamlaka ilizindua mfumo mpya wa uangazi wa hali ya hewa ya anga ya juu katika kituo cha kupima hali ya hewa ya anga ya juu kilichopo JNIA.”amesema

Dk Kabelwa,amefafanua kuwa Mamlaka hiyo iliingia mkataba wa ununuzi wa vifaa na mitambo mbalimbali ya hali ya hewa ikiwemo mitambo nane ya kutoa huduma za hali ya hewa kwa ajili ya usafiri wa anga, mitambo 13 ya kupima hali ya hewa mahususi kwa sekta ya kilimo. Aidha, Mamlaka ilifungua hati ya dhamana (Letter of Credit) ya asilimia 80 kwa ajili ya mitambo hiyo.

Aidha Mamlaka imeendelea kutekeleza jukumu la kutoa utabiri wa hali ya hewa wa kila siku, siku 5, siku 10, msimu na tahadhari ambapo usahihi wa utabiri katika kipindi husika ulikuwa asilimia 93.8 ukiwa juu ya asilimia 70 ya kiwango cha usahihi kinachokubalika kimataifa.

”Huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga ziliendelea kutolewa kwa kuzingatia mfumo wa kudhibiti ubora wa huduma (ISO 9000:2015) ambapo jumla ya ndege 40,323 zilihudumiwa katika mwaka 2021/22 ukilinganisha na ndege 35,111 zilizohudumiwa katika mwaka 2020/21 ambalo ni ongezeko la asilimia 13.”amesema 

Amesema kuwa ongezeko hili linatokana na jitihada za kuifungua nchi zinazofanywa na Serikali yetu pamoja na kuendelea kukidhi viwango vya Kimataifa na kuhakikishia dunia usalama wa anga la Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kwa ndege zote za kimataifa.

Dk Kabelwa ameongeza kuwa kwa upande wa utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa watumiaji wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu Mamlaka kupitia ofisi zake zilizopo kwenye Bandari za Bahari ya Hindi na Ziwa Victoria, Nyasa na Tanganyika inaendelea kutoa huduma kwa ufanisi.

“Huduma hizi zimechangia kuongezeka kwa usalama na ufanisi wa shughuli za kiuchumi zinazofanyika kwenye maji ikiwemo usafiri, shughuli za bandari, uvunaji wa gesi asilia,

Na kuongeza kuwa “Katika mwaka 2021/22, idadi ya watumiaji wa huduma za hali ya hewa kwa sekta ya maji iliongezeka na kufikia 36,774 ikiwa ni ongezeko la asilimia 19 ukilinganisha na watumiaji 32,736 waliohudumiwa katika mwaka 2020/21,”Amesema Dkt.Hamza

Dk Kabelwa amesema kuwa Mamlaka imeendelea kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake iliyopewa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani ya kuwa Kituo cha kutoa mwongozo wa utoaji wa utabiri wa hali ya hewa kwa nchi za ukanda wa Ziwa Victoria (Regional Specialized Meteorological Centre) kwa nchi zilizopo Afrika Mashariki.

“Jukumu lingine la kimataifa ni kusaidia ufuatiliaji wa ubora na upatikanaji wa data za hali ya hewa kwa vituo vya hali ya hewa vilivyo katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, na Sudan ya Kusini kupitia kituo cha Kanda kilichopo Tanzania”

Na kuongeza kuwa “Matukio mbalimbali ya kutopatikana kwa data yaliripotiwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani kwa ajili ya kupata msaada zaidi na pia kiliendelea kutoa ripoti za kila mwezi ambazo zilitumwa kwa nchi za Afrika Mashariki,” amefafanua Dk Kabelwa

Dk Kabelwa amesema wanaendelea na kupanua wigo wa utoaji wa elimu kwa wananchi na wadau wengine juu ya umuhimu wa huduma za hali ya hewa na kuendelea na utekelezaji wa Sheria Na.2 ya mwaka 2019 na Kanuni zake.
 
Pia wataongeza vyanzo vya mapato kwa lengo la kuboresha huduma za hali ya hewa, kuendelea kuboresha miundombinu ya Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa na kuandaa miradi mbalimbali yenye lengo la kupata rasilimali kutoka kwa washirika wa maendeleo ndani na nje ya nchi ili kuboresha huduma za hali ya hewa nchini.

Naye Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa idara ya Habari -MAELEZO Gerson Msigwa,amewataka Wananchi kujenga utaratibu wa kutumia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

“Ni muhimu sana kutumia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kwani ndio zitakazokusaidia siku yako iweje unaweza ukatoka na koti wakati utabiri unaonesha kuwa siku hiyo kutakuwa na jua kali au pengine unaweza kutoka hujavaa sweta kumba siku hiyo kutakuwa na baridi hivyo tujenge utamaduni wa kila asubuhi kabla hujatoka angalia kwanza hali ya hewa itajuaje,”Amesema Msigwa

MKURUGENZI Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Hamza Kabelwa ,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Novemba 2,2022 jijini Dodoma.

MKURUGENZI Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Hamza Kabelwa ,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa  na waandishi wa habari  (hawapo pichani) kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Novemba 2,2022 jijini Dodoma.

About the author

mzalendoeditor